• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 9:16 PM
DOUGLAS MUTUA: Ni vyema kiongozi wa nchi kuwa na mtagusano na raia wake akiwa hai

DOUGLAS MUTUA: Ni vyema kiongozi wa nchi kuwa na mtagusano na raia wake akiwa hai

NA DOUGLAS MUTUA

MOJAWAPO ya mambo yaliyosemwa kimzaha mtandaoni wiki iliyopita nikabaki kuyatafakari ni kwamba, wananchi wa kawaida wanafaa kupewa fursa za kutangamana kwa njia huru na marais kabla hawajatangulia mbele ya haki.

Mkenya wa kawaida aliyesema hili alilalamika kimzaha, japo akimwomboleza Rais Mstaafu Mwai Kibaki, kwamba haifai kwa raia kuruhusiwa tu kumkaribia kiongozi wao akiaga dunia.

Unaweza kuonekana kama mzaha wa kizushi, lakini wachangiaji wengine mtandaoni walikubaliana nao na kupiga mfano wa alivyoombolezwa Rais Mstaafu, marehemu Daniel Moi.

Waliokuweko wakati wa msiba wa mwanzilishi wa taifa, Mzee Jomo Kenyatta, walikuwa na maoni kama hayo pia; kumwomboleza mtu si muhimu kuliko kumkaribia akiwa hai.

Labda ni suala ambalo linaweza kuzingatiwa na kushughulikiwa, wakuu wa itifaki wakahakikisha kiongozi wa nchi, wakati wa utawala wake, ana mtagusano wa kutosha na raia.

Mathalan, majukwaa kadhaa yanaweza kuandaliwa kote nchini kila mwaka, rais akatoa mihadhara ya umma, kisha akaulizwa maswali na mwananchi wa kawaida na akayajibu palepale.

Tunaweza kujaribisha mpango huu kwa kuwa na angaa mkutano mmoja kila wiki kati ya rais na wanahabari wa kiwango cha chini, si wahariri, ambapo masuala ya kimsingi yanayowahusu kina yakhe mashinani yanajadiliwa.

Hiyo itakuwa fursa nzuri ya kumpa rais sifa za binadamu, si mtu mashuhuri na mkali asiyekaribiwa vivi hivi, wala rafiki wa wachache na mtawala wa mamilioni.

Hilo litawezekana tu ikiwa tunajichagulia mtu na akili zake, asiye na hofu yoyote anapojibu maswali ya kushtukiza kutoka kwa wanahabari wazushi na wananchi wajanja.

Ingawa mjadala huo wa mtandaoni ulimweka marehemu Kibaki ndani ya kasha moja na watangulizi wake, binafsi nadhani alikuwa tofauti nao kwa namna nyingi sana.

Nadiriki kusema ndiye aliyekuwa na sifa za binadamu wa kawaida, mtu ambaye unaweza kumfananisha kwa kila hali na mwingine unayemjua, kasoro kuwa rais tu.

Wapo wengi tu ambao walikua na kusoma naye; ndugu zake tunawajua, zipo hata picha za babake, sikwambii zake mwenyewe akiwa kijana, kwenye mazingira mbalimbali.

Hatuwezi kusema haya kuwahusu marehemu Kenyatta na Moi; historia zao zina mapengo mapana, wala hatupati maelezo kamili kuwahusu, na hatuwajui waliosoma nao.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

VITUKO: Chicharito hatarini kutemwa kufuatia ukware wake na...

KCB yamwaga Sh70m kudhamini mbio za magari Uganda

T L