• Nairobi
  • Last Updated December 6th, 2023 9:00 PM
DOUGLAS MUTUA: Uhusiano wa Urusi na Afrika utawaramba Waafrika

DOUGLAS MUTUA: Uhusiano wa Urusi na Afrika utawaramba Waafrika

NA DOUGLAS MUTUA

LAITI pangalikuwapo na mfumo mbadala wa siasa ambapo wananchi wanajiwakilisha moja kwa moja bila kuwachagua viongozi.

Nimesalitika kuliwazia hili kwa kuona jinsi viongozi wa Afrika wanavyovunjika miguu wakikimbia kumkumbatia Rais Vladmir Putin wa Urusi, katili muua watu bila tafakuri.

Hivi huoni aibu kwamba, miezi mitatu kabla ya kongamano la Urusi na mataifa rafiki kufanyika Afrika Kusini, Waafrika wanatishia yeyote anayewaza kumkamata?

Putin ni mtoro wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) anayetafutwa kwa kukiuka haki za binadamu, hasa kuwateka na kuwasafirisha watoto wa Ukraine hadi Urusi.

Mataifa wanachama wa Mkataba wa Roma ulioanzisha Mahakama hiyo yana wajibu wa kumtia mbaroni na kumfikisha ICC mtu yeyote aliyetolewa kibali cha kukamatwa.

Uhusiano kati ya Bw Putin na viongozi wa Afrika haujajikita katika maadili ya kuwafaa wananchi ila katika tamaa ya viongozi hao, naye akipanua ushawishi wa Urusi duniani.

Wazo la watu kujiwakilisha moja kwa moja limenijia kwa kuwa naamini Mwafrika yeyote mwenye akili razini anapaswa kufahamu kuwa uhusiano huo haumfai kitu, ataponzeka.

Kinyume na mataifa mengine makuu duniani kama vile Marekani na yale ya magharibi mwa Uropa, Urusi haina historia ya kutetea haki za wanyonge kokote duniani.

Hii ina maana kwamba Putin hawezi kuwakanya wala kuwazuia marafiki zake wanaoongoza Afrika, wakigeuka makachinja mradi uhusiano wake nao unanawiri.

Mataifa ya Afrika ambayo yamejasiria kujaribisha demokrasia yana uzoefu wa Marekani, Uingereza, Ujerumani na kadhalika zikiingilia kati kila migogoro inapozuka.

Mathalan, haki za binadamu ambazo Wakenya hutetea kwa fujo kila serikali inapothubutu kuzigusa ni wazo ambalo walipewa na Wamarekani na raia wa mataifa hayo ya Uropa.

Aghalabu, suala la haki za binadamu likiibuka, na serikali iwe mshukiwa, inatabirika kwamba marifiki zetu hao watapendekeza haki itendeke.

Wanajua kutafuta uwiano kati ya maslahi yao na utawala wa sheria katika nchi husika, hivyo viongozi wetu hawawezi kujifanyia mambo kwa jeuri na unoko wa kupitiliza.

Hatuwezi kusema hivyo kuhusu Urusi! Putin anahitaji tu kiongozi mlafi aliye radhi kupokea mafedha yake na msamaha wa madeni bila kuwajibishwa na yeyote, basi!

Ikitokea maji yazidi unga katika taifa la kiongozi kama huyo fisadi, na hilo si jambo tukizi Afrika, Urusi itamuunga mkono hata akiwa katili namna gani.

  • Tags

You can share this post!

Sudan: Amerika yatishia kuweka vikwazo vipya

TAHARIRI: Mchango wa Ingwe ni muhimu katika soka

T L