• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
DOUGLAS MUTUA: Usichague wenye ndimi telezi bali unaowaamini

DOUGLAS MUTUA: Usichague wenye ndimi telezi bali unaowaamini

NA DOUGLAS MUTUA

WENZETU kutoka janibu za Mlima Kenya husema anayeendewa ugangani huambiwa chochote. Kisa na maana? Mwenyewe hakwenda kupiga bao ajuaye aliyeenda.

Katika kipindi cha kampeni kinachoisha leo Jumamosi, Wakenya tumeendewa ugangani mara nyingi tu, hivyo nadiriki kusema hatuna lazima ya kukubali wala kuamini tuliyoambiwa.

Kampuni za kura za maoni zimetuzoea sana. Zimezuka za kila aina – za kweli na nyingine hewa, sikwambii na za mtandaoni zisizo na sura – kutabiri Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Jumanne, Agosti 9, 2022.

Kama maporomoko ya maji, zimeshindana kuchapisha matokeo ya tafiti zao na kuwana kutusadikisha eti zinayochapisha yanaaminika.

Na kwa kuwa mihemko ya kisiasa haiishi Kenya, watu nusra wavaane barabarani, kwenye vyombo vya habari na mitandaoni wakibishana kuhusu matokeo hayo.

Yanayoibua hisia kali zaidi ni matokeo kuhusu uchaguzi wa urais; wafuasi wa miungano ya Kenya Kwanza na Azimio la Umoja ndio ambao wameonyesha jeuri katika ubishi huo.

La kushangaza ni kwamba, makundi hayo mawili yanafanya mambo kana kwamba maamuzi yamekwisha fanywa, hayajitahidi kushawishiana wala kusadikishana kuhusu sera.

Wafuasi wa Naibu Rais, Dkt William Ruto, anayewania urais kwa chama cha United Democratic Movement (UDA) chini ya mwavuli wa Kenya Kwanza, wanabishana tu na wale wa Bw Raila Odinga, anayebeba mwenge wa Azimio.

Sababu kuu ni kwamba, Bw Odinga ameibuka kidedea katika matokeo ya tafiti sita kati ya tisa za hivi majuzi zaidi, huku Dkt Ruto akishinda tatu pekee.

Wafuasi wa Bw Odinga hawawezi kutulia kwani wanadhani ameshinda, eti anamsubiri Rais Uhuru Kenyatta afunganye virago, aondoke Ikulu na kumkabidhi ufunguo akitokea mlangoni.

Nao wa Dkt Ruto wanaamini hashindiki hata kwa dawa; kampeni za miaka minne unusu alizofanya kote nchini kuwahamasisha kina yakhe haziwezi kuwa kazi bure, nguvu ya mtu iliwe eti.

Pamoja na mapendeleo yetu, tunafaa kujirudi, tudhibiti hisia zetu, tuyashushe matamanio yetu, tukumbuke bado hatujapiga kura, madebe yatazibuliwa Agosti 9 tupenyeze kura zetu.

Nimesema na nasisitiza: Hatuna lazima ya kukubali wala kuamini matokeo ya kura za maoni. Yana historia yenye utata, si nchini Kenya tu bali pia Marekani.

Kutokana na utabiri wa uongo wa chaguzi tatu kuu zilizopita, madai ya kura kuibwa yamekaririwa mara nyingi hivi kwamba, baadhi ya Wakenya hawana imani na uchaguzi kabisa, wanasadiki utavurugwa.

Uchaguzi ni kama kandanda, mshindi hujulikana baada ya kipenga cha mwisho. Piga kura kana kwamba hujaona kura za maoni, jichagulie unayeamini atakufaa. Ni maisha yako, si yetu.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Haki Africa yazindua kituo cha kufuatilia uchaguzi

Wanaodaiwa kusambaza ujumbe wa uchochezi wapata bondi

T L