• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
JURGEN NAMBEKA: Mafuriko ya Mwatate ishara hatujapangia hali za dharura

JURGEN NAMBEKA: Mafuriko ya Mwatate ishara hatujapangia hali za dharura

NA JURGEN NAMBEKA

TAARIFA za hivi punde za watu kadha kupoteza maisha pamoja na mali ya mamilioni kuharibiwa na mafuriko katika Kaunti ya Taita Taveta, zimeacha wakazi na maswali machungu.

Kulingana na habari za mkasa huo, wakazi walikuwa wamejenga makazi katika kingo za mto uliokaushwa na kiangazi.

Kwa misimu minne mvua haikunyesha na wakaamua kuekeza nyumba zao hapo, wakasahau mto hufuata mkondo wake.

Haya yakijiri, taasisi za kushughulikia hali dharura katika kaunti zilifumbia jicho ujenzi huo, ambao ni wazi ulihatarisha maisha .

Je, wakazi wa Taita Taveta waliamua kujenga nyumba zao kwenye mkondo wa mto bila kufikiria athari ambazo zingetokeza endapo mvua ingenyesha?

Suala ibuka ambalo huenda hata likazua minong’ono siku za usoni, ni iwapo Mamlaka ya Kitaifa ya Kushughulikia Majanga (NDMA), ilituma maafisa wake kuonya wakazi dhidi ya ujenzi huo.

Maisha ya wakazi na mali ya thamani huenda ingeokolewa iwapo NDMA ingetekeleza wajibu wake kutimua wakazi hapo.

Inafedhehesha kuwa ujumbe wa Mbunge wa Mwatate, Bw Peter Shake, wa jinsi ya kuhamasisha watu waliojenga bondeni, umechelewa sana.

Iwapo viongozi wangehakikisha ujumbe huo unatolewa mapema, majanga na hasara iliyokumba wakazi haingekuwepo.

Ila je, ni yapi yanaweza kufanywa ili kuepuka majanga haya kesho na siku za usoni?

Kuna umuhimu gani kuwa na mamlaka ya kupambana na majanga na hata taasisi za dharura, iwapo hazitahakikisha wakazi wako tayari kwa dharura hizo?

Kwanza, licha ya ukame wakazi wanapaswa kuondolewa maeneo hatari na kutafutiwa sehemu nyingine za kuishi ili kuepuka ajali na majanga ya baadaye.

Ni vyema NDMA ielimishe wakazi wa maeneo yenye kuathiriwa na mafuriko na majanga mengine, dhidi ya kurudi sehemu hizo hatari.

Hamasisho la jinsi ya kujikinga endapo utajipata katika janga pia ni muhimu. Kwa sasa mmoja wa wahasiriwa angelikuwa hai iwapo angetoroka na wenzake.

Kwa mujibu wa Naibu Kamishna wa Taita Taveta, mhasiriwa huyo alirudi kujifungia kwa nyumba wenzake wakitoroka.

Hamasisho kuhusu nguvu za maji huenda lingemsaidia kufanya maamuzi ya haraka upesi ambayo yangemfaa kujiokoa.

Pia vikosi vya kushughulikia dharura vinapaswa kuwa ange na tayari wakati wowote kuokoa waathiriwa. Nyingi ya hali za dharura nchini zinatambulika wakati wazo kutokea.

Serikali ya kitaifa na za kaunti zikiendelea kufumbia jicho suala la utayari wa kupambana na majanga, majuto yatatujia.

  • Tags

You can share this post!

Leteni hao Arsenal – Klopp

Raila njiapanda kuhusu muafaka akionekana...

T L