• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 11:39 AM
LEONARD ONYANGO: Pana hatari ya baa la njaa kuzidi changamoto za kilimo zisipokabiliwa

LEONARD ONYANGO: Pana hatari ya baa la njaa kuzidi changamoto za kilimo zisipokabiliwa

NA LEONARD ONYANGO

IDADI ya watu wanaohangaishwa na baa la njaa nchini huenda ikaongezeka maradufu baada ya Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9 iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa kupambana na changamoto zinazokumba sekta ya kilimo wakati huu.

Wakulima wamekumbwa na uhaba wa mbolea, kuchelewa kwa mvua na janga la viwavi (fall armyworm) ambao wamevamia mashamba katika maeneo mbalimbali nchini, hasa kanda za Magharibi na Bonde la Ufa ambazo huzalisha mahindi kwa wingi.

Kuchelewa kwa mvua kulichelewesha shughuli ya upanzi katika maeneo mengi ya nchi.

Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa tayari wiki iliyopita ilisema kuwa mvua inayonyesha sasa itakuwa haba Kaskazini Mashariki, Pwani kati ya maeneo mengineyo.

Kuongezeka kwa bei ya mbolea kumesababisha wakulima wengi kupanda bila bidhaa hiyo muhimu – hali ambayo huenda ikaathiri pakubwa mavuno.

Hatua ya Uturuki kupiga marufuku kuuzwa kwa mbolea yake aina ya Calcium Ammonium Nitrogen (CAN) pia itaathiri pakubwa sekta ya kilimo humu nchini.

CAN hutumiwa baada ya upanzi na tayari wizara ya Kilimo imeonya kuwa kutakuwa na upungufu wa mbolea hiyo humu nchini kufuatia marufuku hiyo ya Uturuki.

Huku wadudu wanaoharibu mazao wakiendelea kuenea kwa kasi katika maeneo mengi ya nchi, serikali za kaunti zinaonekana kulala usingizi wa pono – viongozi wanachapa kampeni za kusaka viti katika uchaguzi ujao bila kujali masaibu ya wakulima.

Serikali ya kitaifa pia inaonekana kujikokota katika kukabiliana na viwavi hivyo ambavyo huenda vikasababishia wakulima hasara kubwa na kutumbukiza mamilioni ya Wakenya katika baa la njaa.

Serikali za kaunti hazina budi kutoa mafunzo kwa wakulima kuhusu jinsi ya kukabiliana na wadudu hao kwa kutumia njia za kiasili.

Kaunti pia zinafaa kununua kemikali zitakazotumiwa kupambana na wadudu hao ili kunusuru wakulima.

  • Tags

You can share this post!

Rangers wadengua RB Leipzig na kufuzu kwa fainali ya Europa...

Wafanyakazi wagoma wakidai malipo yao

T L