• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 5:17 PM
CECIL ODONGO: Msimamo mkali wa Mudavadi huenda ukamsukuma upinzani

CECIL ODONGO: Msimamo mkali wa Mudavadi huenda ukamsukuma upinzani

Na CECIL ODONGO

KUNA kila dalili kwamba, huenda kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi akasalia kwenye baridi ya kisiasa huku vinara wenzake ndani ya OKA wakionekana kujipanga kuungana ama na mrengo wa Naibu Rais Dkt William Ruto au Kinara wa ODM Raila Odinga kuelekea 2022.

Matukio ya hivi karibuni yanaonyesha kuwa, Mabw Kalonzo Musyoka na Gideon Moi huenda washaamua kuungana na mrengo wa Bw Odinga muungano wa OKA ukionekana kuanza kuporomoka.

Seneta wa Bungoma, Moses Wetang’ula naye anaonekana kukabiliwa na maamuzi magumu zaidi kisiasa na upo uwezekano akasalia na Bw Mudavadi au kuunga mkono mrengo wa Dkt Ruto.

Iwapo mwishowe, Bw Wetang’ula na waziri wa zamani Cyrus Jirongo wataamua kumuunga Bw Mudavadi, huenda kusiwe na tofauti kubwa kwa kuwa wawili hao wanatoka eneo moja.

Ziara ya Dkt Ruto na Bw Odinga wiki jana eneo la Ukambani, ilidhihirisha kuwa, eneo hilo lipo tayari kushabikia mmoja wa vinara hao japo mrengo ambao Bw Musyoka atauunga mkono huenda ukavutia kura nyingi zaidi.

Kwa kuwa magavana Charity Ngilu (Kitui), Profesa Kivutha Kibwana (Makueni) na Dkt Alfred Mutua (Machakos) washajiunga na mrengo wa Bw Odinga, lazima Bw Musyoka ajinasue kudumisha umaarufu wake; na hilo ni kwa kuwania urais au kuunga mkono mrengo wa Bw Odinga japo amenukuliwa mara kadhaa akiapa kutofanya kazi tena na waziri huyo mkuu wa zamani.

Japo OKA imekuwa ikisisitiza bado wao ni fungu moja, huenda isiwe rahisi kwa upande wa Bw Musyoka kushawishika kumuunga mkono Bw Mudavadi kwa sababu ngome yake ya Ukambani ina kura nyingi kuliko Magharibi.

Ukambani ina jumla ya kura milioni 1.8 nazo kaunti nne za Magharibi zina kura milioni 2.5 japo Bw Odinga ana uungwaji mkono mkubwa eneo hilo ikilinganishwa na kigogo huyo wa ANC.

Kwa hivyo, itakuwa vigumu kwa Bw Musyoka kuwaeleza wafuasi wake kwa nini atasalimu amri ya kutofika debeni na kumuunga mkono Bw Mudavadi.

Kauli ya Bw Moi akiwa ameandamana na Bw Musyoka kuwa wataunda muungano na mrengo wa Raila/Uhuru inadhihirisha kuwa wamemtaliki Bw Mudavadi kisiasa.

Hali ambayo OKA imejipata sasa ni kama ile ya Ford mnamo 1992 ambapo Jaramogi Oginga Odinga na Kenneth Matiba wote walikuwa wakipigania tiketi ya kuwania urais katika uchaguzi wa kwanza baada ya kukumbatia mfumo wa vyama vingi.

Kwa kuwa Bw Mudavadi ashakata kauli atakuwa debeni, Bw Musyoka anaonekana kutathmini hali na huenda asiwe na jingine ila kubadili nia na kujiunga na kambi ya Bw Odinga kwa kuwa kuna uhasama mkubwa kati yake na Dkt Ruto.

Pigo jingine kwa Bw Mudavadi ambaye ashaamua kuwa hatarudi nyuma kwenye azma yake 2022 ni kuwa, wandani wake ambao wanafaa wamvumishe maeneo mengine, wamekuwa wakiendeleza kampeni magharibi mwa nchi hasa Kakamega pekee.

Seneta wa Kakamega Cleophas Malala na mbunge wa Lugari Ayub Savula wamekuwa wakijikita katika kampeni za kumvumisha Bw Mudavadi, Kakamega ambako wawili hao wanapigania tiketi ya ANC kumenyania kiti cha ugavana.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Mkazi adai hakimiliki za ‘Bottom up’

Utafunaji miraa unaharibu hali ya usafi – Jaji

T L