• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 PM
Mkazi adai hakimiliki za ‘Bottom up’

Mkazi adai hakimiliki za ‘Bottom up’

Na RICHARD MUNGUTI

MFANYABIASHARA aliyebuni mfumo wa kiuchumi wa “Bottom Up” anaomba Mahakama Kuu iwazime wanasiasa kuutumia kama kauli mbiu katika kampeni zao.

Bw Jacob Muting’a Kioko aliyewasilisha kesi hiyo chini ya sheria za dharura anaomba mahakama iwazime Naibu Rais Dkt William Ruto, maafisa wakuu serikalini na wanasiasa kuutumia mfumo huo anaodai aliubuni 2010.

Katika kesi aliyowasilisha katika Mahakama Kuu Milimani, Bw Kioko alisema wanasiasa walitwaa mfumo huu aliouzindua Mei 31, 2013 na kuukabidhi kwa maafisa wakuu serikali waukumbatie katika kuimarisha mapato ya wananchi maskini.

Kioko amewasilisha ushahidi katika mahakama kuu kuthibitisha jinsi aliwaandikia , Rais Uhuru Kenyatta, Dkt Ruto, Waziri wa Ustawishaji viwanda , Spika wa Bunge la Kitaifa na Mwanasheria Mkuu akieleza jinsi serikali inaweza kutumia mfumo huu alioubuni kuwastawisha wakenya wa mapato ya chini.

Bw Kioko amesema badala ya serikali kutekeleza mfumo huu, sasa Dkt Ruto kupitia chama chake cha United Democratic Alliance (UDA) amekuwa akitembea kote nchini akiwaeleza wananchi atatumia mfumo wa “Bottom Up” kufufua uchumi wa nchi hii na kuboresha mapato ya “Mama Mboga , Boda boda na wafanyabiashara wadogo.”

“Miaka mingi imepita tangu niubuni mfumo huu wa “Bottom Up” mnamo 2010 kisha nikaupeana kwa Serikali kuu 2013 uanze kutekelezwa,” asema Bw Kioko.

“Niliwaandikia maafisa watano wakuu serikalini ambao ni Rais, Naibu wa Rais, Waziri wa Ustawishaji Viwanda, Spika wa Bunge la Kitaifa na Mwanasheria mkuu jinsi mfumo huu unavyoweza kubadilisha uchumi wa nchi hii lakini ulipuuzwa,” asema Bw Kioko.

Mlalamishi huyu aliyeshtaki Serikali anasema alibuni mwongozo kwa lugha ya kiutaalam Dichotomous Universal Grown Web Innovation (DUGWI) na ukazinduliwa mnamo Mei 31, 2013.

Bw Kioko anadai chini ya DUGWI mfumo wa “Bottom Up” umepata umaarufu mkubwa na sasa wanasiasa wanaung’ang’ania.

Mfumo huu wa DUGWI Bw Kioko amesema utapeleka kasi masuala ya kiuchumi kwa ushirikiano wa sekta ya kibinafsi na sekta ya umma.

Ushahidi uliowasilishwa mahakani umebaini wanasiasa wasiouelewa mfumo huu wamekuwa wakiwapotosha mamilioni ya wakenya kwamba watautumia katika kujistawisha.

“Wanasiasa wasiouelewa mfumo wa “Bottom Up”wamekuwa wakiwapotosha wananchi. Wale wanaouunga mkono na wanaoupinga hakuna anayeuelewa.Pande zinatapatapa kwenye giza.Hazina ufahamu jinsi ya kutekeleza mfumo huu nilioubuni,” asema Bw Kioko katika ushahidi aliouwasilisha mahakama kuu jana.

Dkt Ruto kupitia kwa chama cha UDA amekuwa akijipigia upatu kwamba atatumia mfumo wa “Bottom Up” kubadilisha hali ya maisha ya wananchi wa mapato ya chini.

Wapinzani wa Ruto haswa viongozi wa chama cha ODM wamemshutumu Dkt Ruto kwa kuwapotosha wananchi akidai ataboresha hali yao ya maisha kupitia mfumo huu wa “Bottom Up”

Kutoeleweka kwa mfumo huu na kupotoshwa kwa wananchi ni tisho kuu hata kwa usalama wa kitaifa ikitiliwa maanani tunaelekea uchaguzi mkuu.

Bw Kioko anaomba mahakama kuu iamuru serikali ikumbatie mfumo huo wake kuimarisha uchumi wa nchi hii badala ya kuachilia wanasiasa kuutumia kama chambo kujipigia debe.

Mlalamishi anaiomba mahakama kuwaagiza wanasiasa wanaoutumia mfumo huo kujipigia debe kumlipa fidia kwa kumwibia hakimiliki.

Pia anaomba mahakama imfidie kwa vile wanasiasa wanajinufaisha na uvumbuzi wake.

You can share this post!

ZARAA: Wakulima wapiga mabroka chenga

CECIL ODONGO: Msimamo mkali wa Mudavadi huenda ukamsukuma...

T L