• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
TAHARIRI: Haki za walemavu zitiliwe maanani kwa CBC

TAHARIRI: Haki za walemavu zitiliwe maanani kwa CBC

NA MHARIRI

KILIO kuhusu utekelezaji wa mfumo wa elimu ya CBC kwa watoto walemavu, kinafaa kuchukuliwa kwa uzito.

Kwa muda mrefu sasa, tumeshuhudia midahalo tele kuhusu mfumo huu wa elimu unaochukua mahali pa 8-4-4.

Mijadala mingi kufikia sasa imehusu gharama ya elimu chini ya CBC, maandalizi ya walimu wanaotekeleza mfumo huo, uwepo wa miundomsingi ya kutosha shuleni, miongoni mwa mengine.

Hata hivyo, hatujaona mengi yakijadiliwa kuhusu utekelezaji wa mfumo huu kwa watoto wanaoishi na ulemavu.

Hatua ya wanaharakati wanaotetea masilahi ya walemavu kujitokeza wazi kutaka wasikike inafaa kuzindua wadau wengine wote wa elimu.

Wanaharakati hao wametaka wazazi ambao wana watoto walemavu wawakilishwe kwenye jopokazi linalotarajiwa kuzinduliwa na serikali kukusanya maoni kuhusu mabadiliko katika sekta ya elimu.

Uundaji wa jopokazi hilo ulitangazwa na Rais William Ruto, ambaye alisema ni kwa nia ya kuboresha utekelezaji wa CBC kwa vile kumekuwa na malalamishi mengi hasa kutoka kwa wazazi.

Jopokazi hilo linalosubiriwa, litahitajika kuwasilisha mapendekezo kuhusu yale yanayofaa kudumishwa, yanayostahili kurekebishwa na pengine yanayotakikana kufutiliwa mbali katika mfumo huo.

Ni muhimu sana walemavu kuwakilishwa katika jopokazi hilo na mtu anayeelewa vyema changamoto ambazo wazazi walio na watoto walemavu hupitia wanapowatafutia elimu.

Tunafahamu fika kuwa, katika baadhi ya jamii, juhudi hufanywa ili kuwajumuisha watoto walemavu pamoja na wenzao katika shule za kawaida ili wasihisi kutengwa.

Hata hivyo, ni muhimu kuwa wadau wa elimu waangazie mahitaji katika shule za watoto walemavu nchini zilizo na maelfu ya wanafunzi, ili kuhakikisha watapata mahitaji yao yote kuendeleza elimu bila matatizo.

Sawa na inavyofanywa katika shule nyingine, inafaa kuwe na rasilimali za kutosha kuwawezesha watoto hawa kupita kutoka mfumo wa 8-4-4 hadi kwa ule wa 2-6-6-3 kwa njia ambayo haitawasababishia hasara kwa njia yoyote ile.

Ni matumaini yetu kwamba wazazi walio na watoto walemavu wataondolewa wasiwasi wao hivi karibuni, na watapewa nafasi mwafaka ya kujieleza wazi na pia mapendekezo watakayotoa yatachukuliwa kwa uzito.

Kwa miaka michache iliyopita, tumeona juhudi zikiekwa katika nyanja mbalimbali hasa katiba iliporekebishwa mwaka wa 2010 ili kuhakikisha walemavu wanapata haki sawa katika jamii.

Kwa msingi huu, hili linafaa kuonekana kikamilifu pia katika sekta ya elimu ili haki sawa ianze kutekelezwa kwa watu wanaoishi na ulemavu wakiwa bado ni watoto.

You can share this post!

Watu 3 wafariki katika eneo la Kirigiti baada ya jengo la...

Usambazaji wa chakula cha msaada waanza rasmi

T L