• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 5:50 PM
Watu 3 wafariki katika eneo la Kirigiti baada ya jengo la orofa kuangukia makazi yao

Watu 3 wafariki katika eneo la Kirigiti baada ya jengo la orofa kuangukia makazi yao

NA SAMMY WAWERU

WATU watatu wameaga dunia mapema Jumatatu baada ya jengo la orofa lililokuwa likiendelea kujengwa kuporomoka na kuangukia nyumba eneo la Kirigiti, Kiambu.

Mama na wanawe wawili walifariki wakipelekwa katika hospitali ya Kiambu Level 5, polisi wamesema.

Kufikia wakati wa kuandaa taarifa hii, Kamishna wa Kaunti ya Kiambu Joshua Nkanatha aliambia Taifa Leo watu saba walikuwa wameokolewa kutoka kwa vifusi vya jengo hilo.

Idadi ya watu isiyojulikana wamekwama katika jengo hilo.

Mapema, Gavana wa Kaunti hiyo, Kimani Wamatangi alibadili mkondo na kufika katika eneo la mkasa.

Mojawapo ya video zilizorekodiwa, Bw Wamatangi ameonekana akisaidia kuondoa vifusi kwa ushirikiano na kikosi chake na wasamaria wema.

“Ondoa hayo mawe ukiyarusha kwingine,” gavana amesikika akielekeza.

Kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii, Wamatangi amethibitisha mkasa huo.

“Habari za kuhuzunisha asubuhi ya leo (Jumatatu). Nikienda ofisini, nimelazimika kubadilisha mkondo na kuelekea Kirigiti, Kiambu ambapo jengo linaloendelea kujengwa limeporomoka,” akaarifu kupitia Twitter, @KWamatangi.

Visa vya majengo kuporomoka Kiambu na baadhi ya maeneo nchini, vimekuwa vikiandikishwa mara kwa mara.

Septemba 2021, jengo moja lililokuwa likiundwa liliporomoka eneo la Kinoo, Kiambu mmiliki akilaumiwa kwa kutozingatia sheria za ujenzi.

  • Tags

You can share this post!

Brigid Kosgei ajiondoa London Marathon kuuguza jeraha

TAHARIRI: Haki za walemavu zitiliwe maanani kwa CBC

T L