• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 10:48 AM
TAHARIRI: Hatima ya kandanda iko mikononi mwa rais mpya ajaye

TAHARIRI: Hatima ya kandanda iko mikononi mwa rais mpya ajaye

NA MHARIRI

UTATA zaidi unaendelea kukumba soka ya Kenya kadiri siku zinaposonga.

Hapo juzi, viongozi wa matawi ya Shirikisho la Soka Nchini (FKF), waliita kikao na klabu zinazoshiriki Ligi Kuu ya KPL nchini kupitia barua.

Kwenye mwaliko huo kwa klabu hizo, ajenda zilizotajwa ni kuhusiana na ratiba ya msimu mpya ya mechi za KPL, mdhamini mpya wa klabu, hatua zilizopigwa kurekebisha katiba ya FKF na pia athari ya mabingwa wa KPL Tusker kutoshiriki ligi kuu.

Ingawa baadhi ya klabu hizo ziko tayari kuitkia mwaliko huo wa Julai 16, kinachofadhaisha mno ni kuhusu jukumu la Kamati Shikilizi iliyoteuliwa na Waziri wa Michezo Novemba mwaka jana hadi Mei mwaka huu ambapo muda wao wa kuhudumu uliongezwa.

Licha ya tangazo hilo kuwekwa wazi kwenye vyombo vya habari, hakuna hata sauti moja iliyosikika kutoka kwao au serikali kuhalalisha au kupinga hatua ya FKF.

Maswali yanayopitapita kwenye akili za mashabiki wengi wa soka nchini ni je, serikali imejiondoa kwenye vita katika yake na FKF?

Je, FKF imechukua nafasi yake iliyotwaliwa na serikali na kuchangamkia jukumu lake kama awali ndipo iweze kushawishi FIFA iondoe marufuku?

Kwa vyovyote vile, wizara ya michezo imetelekeza kabisa wajibu wake kwa spoti hii. Kufikia sasa, serikali ya sasa inapoendelea kuondoka pole pole mamlakani, hakuna lolote linaloonekana kuendelea kukwamua tatizo lililogubika soka nchini. Hii ndio sababu Wakenya wengi wanasubiri uongozi ujao kuweza kufufua mchezo huu wenye ufuasi mkubwa duniani.

Kwenye manifesto yake, Naibu Rais aliahidi kuhakikisha Shirikisho la Soka Dunia (FIFA) imeondoa marufuku iliyowekea Kenya ya kutoshiriki mashidano ya kimataifa ikiwa atachaguliwa rais wa nchi hii hapo Agosti 9.

Ingawa Naibu Rais hakuonyesha wazi vile angefikia hilo, ni wazi kwamba, serikali ijayo ndiyo itakuwa na mamalaka ya kusuluhisha mushkili huu kutegemea na namana inavyothamini spoti hii.

Mbali na mwaniaji Ruto, kuna wanaodhani mpinzani wake Raila Amolo Odinga, aliye ni mpenzi sugu wa soka mbali na kuwa na uzoefu, ndiye atakuwa mwokozi halisi. Ni matumaini ya wadau kuwa atakayechukua usukani atanyorosha spoti hii.

You can share this post!

Sh143b kutumika kwa ujenzi wa miji 3 ya Lapsset

Ruto, Raila sasa waibiana ahadi

T L