• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 7:55 AM
TAHARIRI: KCSE: Mzozo wa usahihishaji usuluhishwe kwa hekima

TAHARIRI: KCSE: Mzozo wa usahihishaji usuluhishwe kwa hekima

NA MHARIRI

MAPEMA wiki hii walimu waliokuwa wakisahihisha mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne (KCSE) katika kituo kimoja Kiambu walidinda kuendelea na shughuli hiyo, wakilalamikia malipo duni.

Hii ni licha ya wao kujitolea kufanya kazi kwa saa nyingi; wakiamka saa kumi asubuhi na kulala saa nne usiku.

Maandamano yao yalipelekea wakuu katika Wizara ya Elimu akiwemo Waziri Ezekiel Machogu, Katibu wa Elimu ya Msingi Dkt Belio Kipsang, Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Kitaifa la Mitihani (KNEC) David Njegere na Afisa Mkuu Mtendaji wa Tume ya Kuajiri Walimu (TSC) Nancy Macharia kuingilia kati.

Lengo la wakuu hao lilikuwa kuzuia walimu husika wasihitilafiane na tarehe ya kutoa matokeo ya KCSE.

Ingawa Wizara inanuia kuhakikisha matokeo ya KCSE yanatangazwa siku iliyoratibiwa au mapema wiki hii, ni muhimu kuzingatia kwamba walimu ni wanadamu ambao wanahitaji kupumzika.

Endapo watatakiwa kujinyoosha zaidi kwa manufaa fulani, ni vyema walipwe fedha zitakazotoshana na kujitolea kwao.

Kwa mujibu wa Wizara ilikuwa vigumu kuongeza malipo ya wasahihishaji hao kwa sababu ya vizingiti vya bajeti.

Pupa ya kutangaza matokeo ya mtihani ndio mojawapo ya chanzo cha malalamishi haya.

Iwapo serikali itapunguza muda wa kufanya kazi, kuna uwezekano wa walimu kutolalamika wanaposahihisha karatasi hizo.

Hakuna haja ya kuharakisha walimu kukamilisha shughuli hiyo, huenda kukasababisha makosa ya usahihishaji.

Katika makosa hayo huenda wanafunzi kadhaa wakakosa alama walizopaswa kupata kihalali, kisa ni uchovu wa walimu.

Kwa walimu ambao wamekuwa wakifanya kazi hiyo ngumu hadi kukaribia kuimaliza, ni vyema wasiwe wepesi wa kugoma kwani migomo huwa na athari kubwa.

Kwa mfano, kuondoka kwa walimu kadhaa kambini hapo jana huenda kukawaacha wenzao waliosalia wakipatwa na uchovu zaidi, ikilinganishwa na hapo awali walipokuwa wote.

Ni ombi letu kuwa Wizara ya Elimu itabadilisha msimamo wake kwa suala la kuharakisha usahihishaji. Licha ya kutaka kuonekana kama Wizara inayowajibika, ni vyema pia kuzingatia walimu wanaofanya kazi hiyo.

Iwapo walimu hao watalazimika kufanya kazi kwa muda mrefu kupita kiasi, ni bora wafidiwe ipasavyo. Tunahimiza pande zote husika zipunguze hamaki na zitafute njia mbadala ya kusuluhisha masula yao.

  • Tags

You can share this post!

Olunga abeba Al Duhail ligini Qatar katika ushindi dhidi ya...

JURGEN NAMBEKA: Serikali, kaunti ziunde mbinu kugeuza...

T L