• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
TAHARIRI: Kenya Power sasa iimarishe uhusiano na wateja wake

TAHARIRI: Kenya Power sasa iimarishe uhusiano na wateja wake

NA MHARIRI

TANGAZO la kampuni ya Kenya Power kwamba imesimamisha kandarasi ya kampuni za kibinafsi kusambaza stima ya kujaza lafaa lifuatiliwe kwa makini.

Kenya Power kupitia notisi kwa wateja, ilitangaza kwamba nambari zilizokuwa zikitumika kununua stima ya mjazo au (tokens) hazitatumiwa tena. Kwamba yeyote anayetaka kujaza stima ya kulipia kabla ya kutumia, anapaswa kutumia nambari ya M-Pesa BayBill 888880 au atumie *977# na kuchagua kunua stima hiyo.

Inaeleza kwamba maajenti waliokuwa wakitumiwa kuuza stima hiyo ya mjazo kwa niaba ya Kenya Power hawatatumiwa tena.

Kwamba wateja hawatamlaumu mtu yeyote iwapo wataendelea kulipia stima kupitia nambari walizozoea, zisizokuwa za Kenya Power.

Tangazo la aina hii kwanza ni zuri kwa sababu hakukuwa na sababu za Kenya Power kutumia na kunufaisha watu binafsi kusambaza stima kwa Wakenya.

Ilivyo kwa sasa hakuna kampuni nyingine yenye jukumu la kusambaza stima kwa wateja isipokuwa Kenya Power.

Ilitarajiwa tangu zamani, iwe na uwezo wa kuwauzia wateja stima, bila kuingia gharama.

Kenya Power ni ya umma na mmiliki halisi ni mwananchi.

Wanaoisimamia wanapaswa kuwa na mikakati ya kuhakikisha wanapunguza gharama ya matumizi, kwa manufaa ya raia.

Lakini tunaposherehekea hatua hiyo, kuna masuala kadhaa yanayohitaji kushughulikiwa kwa haraka.

Kwanza, ni kuendelea kuhamasisha wateja kupitia jumbe fupi kwa simu zao kuhusu mabadiliko hayo.

Serikali imekuwa ikiwatumia watu jumbe kuhusu Covid-19.

Safaricom inawatumia wateja jumbe za kujisajili upya, na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) iliwatumia watu jumbe za kuwakumbusha kushiriki kwenye uchaguzi Agosti 9.

Jumbe za kuwakumbusha wateja wasitume pesa kwa kampuni ambazo kandarasi zao na Kenya Power zilitamatishwa, kutawasaidia kuepuka hasara na kuhadaiwa.

Wateja wanaotumia stima ni watu wa viwango mbalimbali.

Kati yao ni watu wa Juakali, wenye vinyozi na wafanyibiashara wadogo. Watu hawa hutumia pesa chache wanazopata ili kuendeleza biashara zao na kujipatia mapato kidogo. Iwapo hawatapata taarifa kamili na pesa zao ziende kusikostahili, wataathirika kiuchumi.

Pili, Kenya Power pia yapaswa kuimarisha jinsi inavyowashughulikia wateja. Mara kwa mara wateja hupitishwa katika hatua nyingi za kuchosha.

Wakati mwingine simu hujibiwa na sauti tu ambayo humtaka mteja asubiri huku pesa zikiendelea kutumika.

Uhusiano mwema na wateja au kutoa taarifa na kurejesha stima haraka itawafanya wateja wasijutie kurejeshwa kwa Kenya Power.

You can share this post!

Wajackoya sasa amtema naibu wake

Omtatah atoa ushahidi kuonyesha hesabu za Chebukati zina...

T L