• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 11:53 AM
TAHARIRI: Kuongeza ada ya maji kutakwamisha maendeleo

TAHARIRI: Kuongeza ada ya maji kutakwamisha maendeleo

NA MHARIRI

MNAMO Juni 30, 2022 Dkt William Ruto akiwa mwaniaji urais kupitia chama cha United Democratic Alliance (UDA), alizindua manifesto yake katika Uwanja wa Kimataifa wa Michezo wa Moi, Kasarani, Nairobi.

Kwenye manifesto hiyo, Dkt Ruto aliahidi kubadili maisha ya Mkenya akichaguliwa kuwa rais, kwa kuangazia sekta kuu sita.

Kati ya hizo, kuna utoshelezaji wa chakula na miundomsingi.

Kuhusu utoshelezaji wa chakula, manifesto inazungumzia kilimo, ambacho kwa sasa kinategemea maji.

Kenya Kwanza iliahidi kwamba badala ya kutegemea mvua, serikali itachimba mabwawa na kuendeleza unyunyizaji maji mashambani.

Chini ya kitengo cha miundomsingi, ahadi kuu ilikuwa inahusiana na maji. Manifesto hiyo ilitambua kipengee cha 43 cha Katiba kwamba maji ni haki ya kimsingi ya kila Mkenya. Kwamba maji ni kiungo muhimu kwa ustawi wa kilimo na thuluthi mbili ya Wakenya hutegemea kilimo cacha unyunizaji mashambani.

Manifesto hiyo inaahidi kwamba kufikia mwaka 2027, kila Mkenya atakuwa na maji ya kutosha kwa kilimo na matumizi mengine ya kinyumbani.

Aidha Dkt Ruto amenukuliwa mara kadhaa akiahidi kupunguza gharama ya huduma muhimu kama maji na nguvu za umeme.

Kwa hivyo ni jambo la kushangaza kuona kwamba chini ya miezi sita tangu Kenya Kwanza iingie serikalini, tayari imeanza kusahau ahadi zake kuhusu maji.

Wizara ya Maji imewapa ilani wakazi wa kaunti sita kwamba ifikapo kesho kutwa, Februari mosi, wataanza kununua maji kwa ada ya juu.

Ilani hiyo inasema maji yatauziwa wakazi wa Isiolo, Meru, Laikipia, Wajir, Garissa na Marsabit kwa bei ambayo ni mara 900 ya bei ya sasa.

Kaunti hizo zitalazimika kununua maji kwa bei ya Sh5 kwa kipimo cha chini, badala ya senti 50 kwa sasa. Ongezeko hilo linajiri wakati ambao sehemu kubwa ya kaunti husika zimeathiriwa na ukame.

Kaunti hizo zipo kwenye mpaka wa mto Ewaso Ngiro na zimekuwa zikiandamwa na ukame uliosababisha mimea kunyauka na mifugo kufa. Kuongezwa kwa ada hiyo ya maji kutawaumiza sana.

Si vibaya kwa serikali kuongeza bei ya bidhaa kama maji, lakini kufanya hivyo wakati hali ya uchumi ni mbaya kwa wananchi, ni kwenda kinyume na msimamo wake kupitia manifesto.

Iwapo serikali itaruhusu utekelezaji wa ada hizo kwa kaunti zinazokumbwa na ukame, ni nini kitazuia kaunti zilizo na maji ya kutosha kufuata mkondo huo?

Ni kwa nini Kenya Kwanza iliweka ahadi kwa maandishi kwamba watu wangepunguziwa gharama ya maji, kama ilijua hizo zilikuwa ahadi hewa?

  • Tags

You can share this post!

PAUKWA: Ujanja wanusuru Msanii asifutwe kazi na Kaburu

KEN OKANIWA: Miaka 60 ya ushirikiano wa Kenya na Japan...

T L