• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 7:55 AM
TAHARIRI: Kurejea kwa SportPesa afueni kwa klabu za ligi

TAHARIRI: Kurejea kwa SportPesa afueni kwa klabu za ligi

NA MHARIRI

HABARI kuu iliyoibuka wiki hii, kando ya kutangazwa kwa mshindi wa urais katika uchaguzi mkuu uliokamilika, ni kurejea kwa kampuni ya kubeti ya SportPesa.

Baada ya kampeni za kisiasa kwa miezi mingi, kilele kilifikia Jumatatu wiki hii baada ya Dkt William Ruto kutangazwa kuwa Rais Mteule.

Hata hivyo, mpinzani wake mkuu Raila Odinga ameapa kukimbia mahakamani kupinga ushindi huo akilaumu dosari katika hesabu ya kura.

Lakini mahakamani huko huko, mtozaji ushuru KRA ilipata ushindi pale rufaa yake kuhusu kodi dhidi ya kampuni ya bahati nasibu SportPesa kupita na hivyo ikakubaliwa kuzoa takriban Sh1.6 bilioni kutoka kwa kampuni hiyo.

Ni jambo lililojiri wakati ambapo kampuni hiyo imerudishiwa leseni yake ya kuhudumu nchini baada ya kuzimwa kwa miaka kadhaa. Ama kwa kweli, kilikuwa kipindi kigumu mno kwa klabu za ligi kuu ambazo zilikuwa zinategemea ufadhili wa kampuni hiyo.

Mahangaiko waliyopita klabu za Gor Mahia na AFC Leopards baada ya kampuni hiyo kuondoa udhamini ghafla hayasemezeki; wachezaji nao hawakusazwa kwenye songombingo hiyo kwa sababu walikaa miezi mingi bila kulipwa ujira na hata wengine kupoteza matumaini kabisa ya kuendeleza vipaji vyao vya soka.

Ingawa kiini cha kufutiliwa mbali kwa leseni ya kampuni hiyo kilitajwa kuwa mzozo kuhusu ushuru haswa baada ya serikali kuupandisha hadi asilimia 35, mkanganyiko na mahangaiko yaliyozuka baada ya kampuni hiyo kujiondoa ghafla inaonyesha kwamba kwenda mbele kutoka hapa, serikali itahitaji kutafuta njia mbadala ya kusuluhisha mzozo kama huu iwapo inajali soka na talanta za spoti nchini.

Kwanza, si haki kwa serikali kutoa leseni kwa kampuni na kuziruhusu kuanzisha shughuli zao, halafu inaamka siku moja na kubadilisha kanuni kabisa na kuathiri shughuli za wahusika, haswa iwapo hatua hiyo inachukuliwa bila mashauriano ya kina na wadau. Hiyo inatoa dhana ya kuwepo kwa nia fiche kwa sababu wachanganuzi watauliza ni nini haswa kilichobadilika.

Ni kweli kwamba kampuni zinafaa kuendeleza shughuli zake kulingana na sheria zilizoko na zile zitakazotungwa haswa zile zinazobuniwa kujaribu kuzuia au kutatua matokeo hasi yaliyoathiri umma kitabia au kimawazo kama vile kutumia muda wao mwingi kubeti badala ya kusaka riziki za kila siku kwa njia za kawaida.

Lakini sasa ni vyema kwa wahusika kuacha yaliyopita na kuganga yaliyomo na yajayo. Na yaliyomo ni kwamba klabu nyingi zinalilia udhamini na huenda jambo la kwanza kabisa SportPesa inafaa kufanya ni kurudisha udhamini uliokuwepo kwa klabu awali.

You can share this post!

WANDERI KAMAU: Uhuru aige watangulizi wake kwa kumkabidhi...

Uhaba wa unga bado wasumbua mamilioni

T L