• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 10:55 AM
WANDERI KAMAU: Uhuru aige watangulizi wake kwa kumkabidhi mshindi uongozi

WANDERI KAMAU: Uhuru aige watangulizi wake kwa kumkabidhi mshindi uongozi

NA WANDERI KAMAU

BAADA ya Mzee Mwai Kibaki kuibuka mshindi kwenye uchaguzi wa urais uliofanyika mnamo 2002, si wengi waliamini ikiwa Rais Daniel Moi angekubali kumkabidhi mamlaka.

Tashwishi hiyo ilitokana na baadhi ya kauli za marehemu Moi, kuwa utawala wa Kanu ungeendelea nchini kwa zaidi ya miaka 100.

Hata hivyo, Bw Moi aliishangaza dunia nzima alipokubali kumkabidhi uongozi Bw Kibaki bila vikwazo vyovyote.

Hali hiyo ilijirudia mnamo 2013, wakati Mzee Kibaki alimkabidhi mamlaka Rais Uhuru Kenyatta bila vikwazo vyovyote, baada ya muungano wa Jubilee kuibuka mshindi.

Sawa na 2002, tashwishi kuu iliyokuwepo 2013 ni jinsi Rais Kenyatta na Naibu Rais William Ruto wangeiongoza Kenya, ikizingatiwa walikabiliwa na mashtaka ya uhalifu wa kivita katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) jijini The Hague, Uholanzi.

Licha ya taswishi hizo, Rais Kibaki aliwakabidhi wawili hao uongozi bila tatizo lolote.

Vivyo hivyo, wito mkuu kwa Rais Kenyatta ni kuwaiga watangulizi wake wawili, kwa kumkabidhi uongozi yule atakayethibitishwa kuwa kiongozi mpya wa nchi baada ya mchakato wa mahakama kukamilika.

Kenya ni taifa linalochukuliwa na dunia nzima kama kati ya mataifa machache barani Afrika ambayo yamekuwa yakizingatia demokrasia kwenye uendeshaji wa taratibu zake za uongozi.

Hivyo, itakuwa vyema kwa Rais Kenyatta kumkabidhi yule atakayethibitishwa kuwa kiongozi mpya, kwa kuwa hatua hiyo ndiyo itaendeleza sifa ya Kenya kama kitovu cha demokrasia Afrika.

  • Tags

You can share this post!

DOUGLAS MUTUA: Ruto apalilie utangamano wa kitaifa akiingia...

TAHARIRI: Kurejea kwa SportPesa afueni kwa klabu za ligi

T L