• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 4:23 PM
TAHARIRI: Mashindano ya Kip Keino ni faida kuu kwa taifa letu

TAHARIRI: Mashindano ya Kip Keino ni faida kuu kwa taifa letu

NA MHARIRI

RIADHA ni mojawapo ya njia ambazo zimepata kuundia Kenya sifa kimataifa kando na kuukuza uchumi wake.

Nchi hii itakuwa na fursa nzuri wikendi hii kupitia mashindano ya riadha ya Kip Keino Classic na Uhuru Classic Nairobi Marathon.

Kip Keino, ambayo itafanyika Kasarani, imevutia baadhi ya wanariadha wazuri na maarufu kabisa duniani wakiwemo mabingwa Marcell Jacobs kutoka Italia (mita 100 Olimpiki), Shelly-Ann Fraser-Pryce kutoka Jamaica (mita 100 duniani) na Peruth Chemtai (mita 3,000 kuruka viunzi na maji Olimpiki (Uganda).

Pia, kuna Norah Jeruto (Kazakhstan), Ismail Ibrahim (Djibouti), Hillary Yego (Uturuki), Ezekiel Mutai (Uganda), John Koech (Bahrain), Samuel Bariso Dugina (Ethiopia), Christine Mboma (Namibia) na Isaac Makwala (Botswana).

Hii ni bila kusahau Waamerika Fred Kerley, Isiah Young na King Kyree, warushaji mkuki matata Ihab Abdelrahman kutoka Misri na Leandro Ramos (Ureno).

Kuna wanariadha stadi wa mchezo wa “Hammer Throw” kutoka Poland akiwemo bingwa wa Olimpiki, Anita Wlodarczyk.

Kenya pia imevuna sifa nyingi kwa kuwa na wanariadha waliopeperusha vyema bendera ya taifa. Mshikilizi wa rekodi ya Afrika mbio za mita 100 Ferdinand Omanyala ni mmoja wa vivutio Kip Keino Classic.

Uhuru Classic itafanyika siku itakayofuatia Mei 8 kwenye barabara mpya ya Nairobi Express Way. Washindi 20 wa kwanza hapo watatia kibindoni kitu kubwa kikiwemo kitita cha Sh6.9 milioni kwa mshindi wa wa kwanza.

Nairobi Marathon, ambayo Waziri wa Michezo Amina Mohamed alisema inalenga kufikia viwango vya mashindano ya haiba kama London Marathon, Berlin Marathon, New York Marathon, Boston Marathon, Tokyo Marathon na Chicago Marathon, imevutia raia kutoka Kenya, Ethiopia na Eritrea, miongoni mwa mataifa mengine.

Huku juhudi za waziri Amina zikitambuliwa kwa kufanukiwa maandalizi ya mashindano haya ya haiba nchini, ni haki kuwapongeza wanamichezo wa taifa hili kujenga msingi ambao umefanya dunia nzima kuitambua nchi hii.

Ni kupitia kwa bidii za wenye vipawa mbalimbali ambapo wanaspoti hao mashuhuri wameamua kututembelea.

Ni dhahiri mikusanyiko kama hii inazidi kuuza nchi yetu kote duniani ambapo sekta ya utalii itazidi kupanuka na kuimarisha uchumi wetu.

You can share this post!

TUSIJE TUKASAHAU: Rais afahamu IDPs wangali wanahangaika

Sonko aanza ngoma Mombasa

T L