• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 3:46 PM
Sonko aanza ngoma Mombasa

Sonko aanza ngoma Mombasa

NA WINNIE ATIENO

KINARA wa Wiper Bw Kalonzo Musyoka amekana madai kwamba ananuia kuvuruga kura za mwaniaji wa Urais kupitia muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya Bw Raila Odinga kwa kumshurutisha aliyekuwa Gavana wa Nairobi Mike Sonko kuwania ugavana wa Mombasa.

Bw Musyoka ambaye ameanza ziara rasmi kaunti ya Mombasa kumzindua Bw Sonko alimpigia debe akisema ni kiongozi wa amani na maendeleo.

“Wengine wanasema Kalonzo anamharibia Baba kura, tungeachilia Bw Sonko aende kwa UDA ingekuwaje? Hii ndio njia mwafaka ya kumsakia Bw Odinga kura, nilitathmini nikaona huu tu ndio mkondo maalum wa kufuata. Bw Sonko ametoka mazingira ya uchochole hadi hapa,” alisema.

Wiki iliyopita, viongozi wa ODM wakiongozwa na mwaniaji wa ugavana wa Mombasa Bw Abdulswamad Nassir alidai kuwa Bw Sonko alitumwa Mombasa na Bw Musyoka ili kuharibu kura za Bw Odinga.

Bw Nassir alimuonya Bw Musyoka dhidi ya kusambaratisha muungano wa Azimio la Umoja One Kenya.

“Wacha kuingilia siasa za Mombasa kwa kumsukuma Bw Sonko Mombasa. Mwezi mmoja hivi uliopita nilisafiri na Bw Sonko na hakunieleza kuwa ananuia kugombania kiti hiki. Lakini juzi alitangaza kuwa ni Bw Musyoka ambaye alimshurutisha kunyemelea siasa za Mombasa. Kama ana haja sana na Mombasa, si angelikuja mwenyewe? Mbona atumane,” alisema Bw Nassir.

Wakati huo huo, Bw Sonko alimsihi Bw Odinga kumchagua Bw Musyoka kuwa mgombea mwenza wake.

Bw Sonko alisema Wiper inamuunga mkono mgombea wa urais wa Azimio la Umoja One Kenya Bw Raila Odinga.

“Tunakupenda na tunakupa heshima, tatizo kubwa ni hao watu wamekuzunguka lakini hatuna shida na wewe. Nilikuwa mwanachama wa ODM, nilipokuwa nikitaka kugombea ubunge wa Makadara nilienda kwa Bw Odinga kumsihi anisaidie hata Mama Ida Odinga na marehemu kijana wake Fidel walikuwa. Baba alikataa niende mchujo na Bw Reuben Ndolo nikawaangusha na kushinda uchaguzi huo mdogo,” alisema Bw Sonko.

Akiongea kwenye ziara yake huko Voi, Bw Sonko alisisitiza ni sharti Bw Musyoka awe mgombea mwenza wa Bw Odinga.

“Usidanganywe, Bw Musyoka ndiye anayefaa na mtashinda. Kwenye siasa za Mombasa hatutajibu matusi waliyoanza. Miaka 10 Mombasa bado wakazi wana changamoto za maji ilhali tumezungukwa na maji ya bahari. Nikishinda nitasafisha maji ili kila mkazi apate maji,” alisema.

Bw Sonko alimshutumu Gavana Hassan Joho kwa kushindwa kukabiliana na utovu wa usalama hasa vijana wanaobeba silaha butu kuvamia wakazi suala ambalo limekuwa donda sugu.

“Umewafanyia vijana maendeleo gani miaka 10 uongozini wewe Bw Joho? vijana wamejiingiza kwenye uhalifu sababu ya ukosefu wa ajira. Mombasa kuna shida kubwa sana na nikiingia nitahakikisha hao vijana wanarekebika tabia na kuwafungulia ajira,” alisema Bw Sonko.

Alionya viongozi wa Mombasa dhidi ya kueneza siasa za ukabila.Alisema ulanguzi wa dawa za kulevya bado ni suala nyeti Mombasa huku vijana wakiendelea kuzama kwenye mihadarati.

“Nitawapeleka vijana vituo vya kurekebisha tabia na kuwatafutia kazi, maskini hawatalipa kodi sababu wameteseka sana sababu ya janga la corona. Tumekuja kukomboa Pwani. Hatutakubali kuitwa bara na ukabila, tuache uadui mdogo mdogo,” alisema Bw Sonko.

Hii leo Jumamosi Bw Musyoka anamzindua Bw Sonko kwenye mkutano wa siasa wa Wiper katika uwanja wa Tononoka ambapo wakuu wa chama hicho watakapoanza rasmi kampeni yao ugavana.

Bw Musyoka alisema mihadarati ni changamoto kwa vijana Mombasa akisisitiza kuwa Bw Sonko ataweka mikakati ya kuwapa nasaha waraibu na kuwapa ajira.

“Wengi wanaanza kuwa na msongo wa mawazo sababu ya uraibu wa mihadarati. Bw Sonko anapenda amani na atahakikisha inadumishwa Mombasa. Wale wanasema ninamharibia Bw Odinga kura wanadanganya, ama mlikuwa mnataka aende UDA?” alisema.

Mgombea wake mwenza ambaye pia ni Mbunge wa Kisauni Ali Mbogo alisema muungano wao ndio unaoweza kuleta mabadiliko.

“Tupende tusipende lazima tubadilishe uongozi wa Mombasa. Gavana Hassan Joho hatakubali kuachilia lakini tutanyakua uongozi kwa mapenzi ya Mungu, nina imani. Nilipoona hawa mabwana wameungana nilijua walikuwa wanatulenga sisi. Wameweka njia zote kutuzuia lakini nyinyi ndio jeshi langu,” alisema Bw Mbogo.

Bw Mbogo alisema yeye ni jasiri na haogopi. Alisema ataendelea kutetea wakazi wa Mombasa.

“Hatuna vita na watu wa tabaka lolote wala kabila yoyote vita vyetu ni kumaliza mabepari wa Mombasa tuwazike katika kaburi la sahau. Hatuwezi kuendelea kunyanyaswa au kudhulumiwa,” alisema.

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Mashindano ya Kip Keino ni faida kuu kwa taifa...

Ruto ameingia baridi – Mucheru

T L