• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 3:13 PM
TAHARIRI: Mawaziri wapigwe msasa bila miegemeo

TAHARIRI: Mawaziri wapigwe msasa bila miegemeo

NA MHARIRI

RAIS William Ruto pamoja na mrengo wake wa Kenya Kwanza amekuwa katika mstari wa mbele kuhakikisha kuwa anadhibiti bunge la kitaifa.

Juhudi hizo zilianza na uteuzi wa aliyekuwa seneta wa Bungoma, Bw Moses Wetang’ula kuteuliwa spika wa bunge la Kitaifa.

Rais Ruto pia alihakikisha kuwa baadhi ya wabunge waliochaguliwa katika mrengo wa mgombea urais wa Azimio-One Kenya, Bw Raila Odinga, wamehamia upande wake.

Mwishoni spika huyo wa bunge la kitaifa alitangaza mrengo wa Kenya Kwanza kuwa ndio wenye wengi bungeni.

Juhudi hizi zinaashiria kuwa, kuna uwezekano wa mawaziri wateule katika serikali ya Rais kuwa na wakati rahisi katika mchakato wa kuwapiga msasa.

Kwa kuwa tayari chama cha UDA ndicho chenye wabunge wengi, kuna uwezekano wa kutowapitishia kwenye mchujo ipasavyo.

Kabla ya mchakato wa kamati ya uteuzi wa mawaziri kuanza kazi yake, mawaziri wateule katika serikali ya Dkt Ruto waliondolewa vizuizi ambavyo vingewazuia kuidhinishwa.

Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma, Bw Noordin Haji aliwaondolea mawaziri wateule Aisha Jumwa na wengine kadhaa mashtaka, na kuwaacha Wakenya wakijisaili maswali kuhusu uhuru wa ofisi yake.

Rais Ruto huenda akawa ‘alilipa’ kujitolea kwao kumsaidia alipokuwa akizozana na rais mstaafu Uhuru Kenyatta, ila ni bora iwapo bunge litamakinika kuwaweka katika mizani mawaziri hao wateule.

Aidha, bunge la kitaifa litapaswa kukubaliana au kupinga ripoti itakayowasilishwa kwake kwa msingi wa ufaafu wa mawaziri hao wala sio umaarufu wao kisiasa. Iwapo ufaafu hautafuata, basi Wakenya wataumia katika mikono ya viongozi wasio na uwezo wa kuwatumikia ipasavyo.

Ili kuepuka malalamishi na ripoti mbaya ya wizara mbalimbali, ni jukumu la kila mbunge kujitenga na upande wanaoegemea kisiasa na kuwateua mawaziri kulingana na uwezo wao.

Mawaziri ambao hawana uwezo wa kutekeleza majukumu yaliyowekwa katika wizara zao, wakataliwe hata kama wabunge wanaoegemea mrengo wa chama tawala ni wengi bungeni.

Kwa wakati uo huo, wabunge wa mrengo wa wachache wanapaswa kuwakubali bila kupinga, wale walio na uwezo wa kutekeleza majukumu waliotengewa katika wizara ambazo wameombwa kutumikia.

Wabunge hao wanapaswa kujitolea kwa hali na mali kuwatumikia Wakenya.

Ni ushauri wetu kuwa, wakati huu wanafaa wajitenge na mirengo yao ya kisiasa kwa ajili ya Mkenya ambaye anahitaji waziri atakayeitumikia nchi.

Ni wakati wa wabunge kukaza kamba na kuwakataa mawaziri wasiofaa, kwa manufaa ya Wakenya waliowachagua na siyo mirengo ya kisiasa.

You can share this post!

Jumwa leo mizanini

Faida za mbegu za katani

T L