• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 1:14 PM
TAHARIRI: Mwaka mmoja wa pata potea: Rais aanze kibarua sasa

TAHARIRI: Mwaka mmoja wa pata potea: Rais aanze kibarua sasa

NA MHARIRI

LEO, Serikali ya Kenya Kwanza inapoadhimisha mwaka mmoja tangu iingie mamlakani, pana haja ya maafisa mbalimbali katika utawala wa sasa kutafakari kuhusu mustakabali wa Kenya.

Kulingana na hali kamili ilivyo pamoja na matokeo mbalimbali ya utafiti, Wakenya hawajaridhika na hatua iliyopigwa na serikali hii.

Rais William Ruto aliahidi mengi wakati wa uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022 lakini mambo yamekuwa kinyume huku uhalisia ukianza kudhihiri.

Dkt Ruto aliahidi vijana kazi, akaahidi kupiga jeki biashara hasa ndogondogo, kuhakikisha huduma bora zinatolewa, kukomesha ukopaji wa kiholela na kumaliza janga la njaa na umaskini uliokithiri.

Hata hivyo, ni bayana kuwa Wakenya wengi kwa sasa wanapitia maisha magumu zaidi kuliko waliyopitia kabla ya utawala wa Kenya Kwanza kuingia enzini.

Hata ingawa baadhi ya wakulima nchini wamevuna mahindi ya kwanza yaliyopandwa hasa kwa kutumia mbolea ya bei nafuu, pakiti ya kilo mbili za unga wa mahindi bado inauzwa kwa zaidi ya Sh200.

Kwa sababu hiyo, familia nyingi zimekuwa zikishinda njaa baada ya kupunguza idadi ya mlo.

Kwa jumla, bei za bidhaa za kimsingi zingali juu, hali inayovuruga maisha ya wengi.

Kuhusu ajira kwa vijana, hakuna hatua yoyote ya uhakika iliyochukuliwa na serikali ili kuwasaidia Wakenya kupata kazi. Kazi za ujenzi zinazotarajiwa kutokana na mpango wa nyumba za bei nafuu si endelevu.

Serikali inafaa kuwazia ufufuzi wa viwanda na kuboresha mazingira kwa wawekezaji wa kigeni kama mkakati madhubuti wa kubuni nafasi za kazi kwa mamilioni ya Wakenya wasiokuwa na njia za kujipa riziki ilhali wana uwezo wa kuchapa kazi.

Vile vile, Rais aliahidi kuhakikisha kila Mkenya, bila kujali uwezo wake wa kifedha, anamudu matibabu kupitia bima ya kitaifa ya afya (NHIF).

Kwa sasa pamekuwepo utata wa malipo ya bima hiyo ambapo hospitali na vituo vingi vya afya vimekataa kutoa huduma kwa wagonjwa hadi serikali iwalipe malimbikizi ya madeni yao.

Pia Dkt Ruto ameghairi nia na kusema kuwa ili Mkenya yeyote anufaike na mpango wake mpya wa huduma za afya, sharti ajisajili na kulipia bima.

Uhalisia ni kuwa Wakenya wengi hawawezi kumudu malipo ya bima, hata yakiwa ni Sh100, sahaulia mbali Sh500 kila mwezi.

Mswada wa Kenya Kwanza wa Bima ya Afya, aidha, unaweza kuwafilisisha raia wengi hasa walioajiriwa iwapo asilimia 2.75 ya mshahara wao itakatwa.

Inakubalika kuwa kipindi cha mwaka mmoja ni kifupi kupima utendakazi wa serikali.

Ndiyo maana Wakenya wako radhi kuusahau mwaka mmoja wa Dkt Ruto enzini, ila kwa ‘sharti’ moja; matokeo mazuri ya utawala wake yaanze kuonekana upesi iwezekanavyo.

Ni wakati wa kutekeleza ahadi za kuboresha maisha ya Wakenya wala si siasa na vijisababu.
Mshindi wa uchaguzi mkuu ujao utaamuliwa na matokeo ya sasa.

  • Tags

You can share this post!

Jinsi walinzi wa vigogo walivyochomoa bunduki na kurushiana...

Tanzania yakana madai ya ulanguzi wa wanyamapori kutoka...

T L