• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 1:15 PM
Jinsi walinzi wa vigogo walivyochomoa bunduki na kurushiana makonde Bomas

Jinsi walinzi wa vigogo walivyochomoa bunduki na kurushiana makonde Bomas

NA SAMWEL OWINO

BUNDUKI zilichomolewa na walinzi wa watu mashuhuri wakirushiana makonde katika ukumbi wa Bomas of Kenya muda mfupi kabla ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi wa urais mnamo Agosti 15, 2022.

Hayo yakiendelea, aliyekuwa Naibu Rais William Ruto, sasa Rais, alitoa amri kali kwa mwenyekiti wa zamani wa Tume ya Uchaguzi (IEBC) Wafula Chebukati amtangaze kama mshindi kwani aliamini ndiye aliyeshinda uchaguzi huo uliofanyika Agosti 9, 2022.

Kimsingi, visanga, ghasia na hata mapigano, miongoni mwa makundi pinzani, yalitokea katika ukumbi wa Bomas na vyumba vya mikutano saa chache kabla ya Dkt Ruto kutangazwa rais mteule.

Kufikia saa tatu za asubuhi Jumatatu Agosti 15, jumla ya meza 15 kwenye ukumbi wa huo hazikuwa na shughuli nyingi, ishara kuwa IEBC ilikuwa inakaribia kutangaza matokeo.

Dakika 10 baadaye, maafisa wa IEBC na maafisa wa usalama walianza kuondoa vitu kwenye meza hizo zilizotumiwa kuthibitisha matokeo, shughuli iliyoendeshwa na maajenti wa wagombeaji urais na wasimamizi wa uchaguzi.

Wakati huu, hakuna aliyejua mshindi wa urais kwani skrini kubwa zilizotundikwa ukumbini hazikuwa zikionyesha idadi ya kura zilizozolewa na wawaniaji 4 wa urais, kila wakati ilivyokuwa awali.

Hesabu za kura ziliwekwa kwenye skrini hiyo mara mbili pekee Jumamosi Agosti 13; saa nne na dakika 43 asubuhi (10.43am) na saa saba na dakika tatu mchana (1: 03pm).

Hesabu hizo hazikuonekana tena.

Makamishna waliokuwa wakisoma matokeo kwa zamu waliulizwa kuhusu kukomeshwa kwa upeperushaji wa hesabu za matokeo kupitia skrini, lakini wakajibu hivi “tutashughulikia suala hilo”.

Mara mbili ambapo hesabu za kura ziliwekwa kwenye skrini, mgombeaji wa Azimio Raila Odinga alikuwa kifua mbele kwa kura chache dhidi ya mpinzani wake mkuu, Dkt Ruto.

Saa nne na dakika 43 (10:43am), Bw Odinga alikuwa na kura 2,061,909 hali Dkt Ruto alikuwa na kura 1,708,801.

Saa saba na dakika tatu za mchana siku hiyo, Bw Odinga aliendelea kuwa mbele kwa kura 2, 288,315 hali Dkt Ruto pia alikuwa amepanda hadi kura 2,036,795.

Hata hivyo, mnamo Jumatatu Agosti 15, viongozi wa kisiasa kutoka mirengo ya Kenya Kwanza na Azimio, ambao tayari wamepata ushindi katika nyadhifa zao pamoja na waliopoteza walianza kuwasili katika ukumbi wa Bomas kila kundi likionyesha matumaini ya wagombeaji wao wa urais kupata ushindi.

Mnamo saa saba, IEBC ilituma taarifa ya kuwaalika wagombeaji urais kwamba ingetangaza matokeo ya mwisho saa tisa alasiri (3pm). Hata hivyo, hilo halikufanyika kwani taifa lililazimika kusubiri kwa saa tatu zaidi.

Mwendo wa saa nane za alasiri, baadhi ya viongozi wa kidini wakiongozwa na Askofu Mkuu wa Kanisa la Kianglikana nchini (ACK) Jackson ole Sapit waliwasili Bomas na kuelekezwa eneo la watu mashuhuri (VIP Lounge).

Walifanya mkutano mfupi na Bw Chebukati kabla ya kuelekea ukumbini.

Wakati huo kuliibuka mgawanyiko mkubwa miongoni mwa makamishna huku hali ya taharuki ikitanda.

Makamishna wanne, wakiongozwa na naibu mwenyekiti, wakati huo, Juliana Cherera walipinga matokeo ambayo Chebukati alitaka kutangaza na tayari walikuwa wameanza kuondoka Bomas.

Viongozi wa kidini hawakuwa na muda wa kuwatuliza.

Walielekea mkahawa wa Serena kuwahutubia wanahabari na baadaye siku hiyo Chebukati na makamishna wawili waliosalia wakamtangaza Dkt Ruto kama mshindi.

Iliripotiwa kuwa Bw Chebukati pia aliwazuia maafisa kadhaa wa Azimio kuona matokeo ya mwisho, licha ya kwamba alishinda akiwaambia mambo yalikuwa shwari.

Baadaye maajenti wa Bw Odinga wakiongozwa na Saitabao ole Kanchory waliitwa kutia saini matokeo ya mwisho.

Walishtuka na kudai kuwa hesabu hizo hazikuwa sahihi kwa kuwa kura kutoka maeneobunge kadhaa zilijumuishwa katika hesabu ya mwisho na mwenyekiti bila wao kupewa nafasi ya kuyakagua.

Bw Kanchory na viongozi wengine wa Azimio waliwahutubia wanahabari nje ya kituo cha habari na kusema kuwa Bw Odinga hatakuja Bomas hadi wakague matokeo ambayo Bw Chebukati alikuwa akielekea kutangaza.

Ndani ya ukumbi mmoja wa maafisa wa Azimio, mmoja wao alikuwa akipiga simu akiuliza mahali kilipo kiti cha Bw Odinga, akisema alikuwa karibu kuwasili.

“Wapi kiti cha Jakom (Odinga), sikioni na mwajua kuwa yu karibu kuwasili,” afisa huyo akasema huku kwaya ikiendelea kutuliza umma kwa nyimbo za Kikristo.

“Kufikia sasa hatujui mshindi. Maafisa wa Azimio wakifanya mkutano nao wanawaambia wao ndio washindi. Wanawapa ujumbe sawa na huo washindani wetu,” akasema mbunge mmoja kutoka Nyanza anayehudumu muhula wa pili.

Dakika chache baada ya saa nane alasiri, maafisa kutoka afisi ya Naibu Rais waliwasili Bomas, ishara kwamba bosi wao alikuwa karibu kufika.

Baada ya maafisa wa Azimio kung’amua kuwa hali haikuwa nzuri kwao, kwani hawakuwa wakipata habari sahihi kuhusu matokeo, mmoja baada ya mwingine waliingia katika magari yao na kuondoka Bomas.

Nje ya chumba ambako Bw Chebukati na maafisa wake walikuwepo, kulikuwa na msukumano wa maafisa wa polisi wenye mavazi ya kiraia.

Maafisa wa usalama wa IEBC walijaribu kumsaidia Bw Chebukati na maafisa wake wafike ukumbini lakini walizuiwa na maafisa wa DCI na maafisa wengine waliovalia mavazi ya kiraia.

Hali hii iliwakanganya maafisa kutoka kwa vikosi vingine vya polisi.

Ndani ya chumba ambako Chebukati alikuwepo alimwagiza afisa wa kisheria wa IEBC Chrispine Owiye asome kipengele cha 138 cha Katiba kinachosema kuwa tume hiyo itajumuisha kura za urais na kutangaza mshindi.

Baada ya Owiye kumaliza kusoma, mwenyekiti huyo alitangaza kuwa mgombeaji aliyeshinda akikuwa “William Ruto.”

Bw Chebukati aliwasomea maajenti kifungu hicho na kuwaagiza watie saini Fomu 34C, inavyohitajika kisheria.

Maajenti wa wagombea urais wote walitia saini fomu hiyo isipokuwa wale wa Bw Odinga.

Bw Kanchory alilalamikia shughuli hiyo na kudai kuwa kulikuwa na njama ya wizi wa kura.

“Hatutakuruhusu kutangaza matokeo haya,” Bw Kanchory akasema akiondoko chumbani humo akiandamana na Seneta wa Narok Ledama Ole Kina.

  • Tags

You can share this post!

Mashabiki wasifu Wahu na Nameless kudumu pamoja licha ya...

TAHARIRI: Mwaka mmoja wa pata potea: Rais aanze kibarua sasa

T L