• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 5:07 PM
TAHARIRI: Raia atazidi kuumia bila ukomavu wa kisiasa

TAHARIRI: Raia atazidi kuumia bila ukomavu wa kisiasa

NA MHARIRI

MATUKIO ya kisiasa yanayoendelea kushuhudiwa nchini yanazidi kuthibitisha kuwa, raia bado hatiliwi maanani sana katika mipangilio ya siasa za kitaifa.

Kwa wiki kadha sasa, mijadala tele imekuwepo kuhusu makubaliano ndani ya miungano mikuu ya kisiasa.

Baadhi ya vyama vimekuwa vikilalamikia kutengwa katika mipango ya miungano hiyo licha ya kuwa na mikataba ya maelewano.

Hata hivyo, kinachojitokeza kadri na jinsi siku zinavyosonga ni kuwa wanasiasa wanapigania maslahi yao ya kibinafsi.

Tunaelewa kuwa, mwanasiasa hutakikana kupigania nafasi yake ndipo apate mamlaka atakayotumia kutetea wananchi. Lakini inavyoonekana, kukurukakara nyingi kwa sasa hazina nia njema kwa mwananchi wa kawaida.

Mienendo ya wanasiasa kukosa misimamo thabiti ya sera wanazodai kuziamini haisaidii maendeleo ya nchi.

Kenya inahitaji ukomavu wa kisiasa kwa kiwango cha kuwa wanasiasa watasimama imara kwa sera zinazolenga kuleta maendeleo kwa wananchi.

Haieleweki jinsi ambavyo kiongozi wa kisiasa hii leo atakuwa akimkashifu mwenzake kwa madai kuwa ni mfisadi, muuaji, asiyejali maslahi ya wananchi na mkosefu wa sera bora za uongozi kisha tunapoamka kesho, wameshikana mikono pamoja wakidai wameona mwangaza bila kufafanua jinsi uswahiba wao mpya utavyookoa mwananchi wa kawaida kutokana na masaibu yake.

Wakati huu viongozi wengi tulionao hutapatapa wakijitafutia makao ya kisiasa yanayoweza kuwatimizia maslahi yao ya kibinafsi, huku wananchi wakiendelea kuteseka.

Changamoto nyingi zinazokumba wananchi tangu jadi hazitaweza kutatuliwa ikiwa tutaendelea kuwa na aina hii ya viongozi wasio na ari ya kutumikia raia.

Masuala kama vile ufisadi, huduma duni za afya, ukosefu wa chakula cha kutosheleza mahitaji ya wananchi, ukosefu wa maji safi nyumbani, miongoni mwa mengine ni mambo ambayo yatazidi kutatiza taifa hili kama hatutapata viongozi wenye maono na misimamo thabiti.

Licha ya kuwepo kwa sera na sheria tele bora ambazo zinafaa kutoa mwelekeo kuhusu utatuaji wa baadhi ya masuala hayo, kile kinachokosekana ni uongozi bora.

Mojawapo ya sababu zinazotunyima uongozi bora ni mienendo hii ya wanasiasa kukosa kuwa na msimamo kwa kiwango cha kupumbaza wananchi kuwa wanawapeleka kulia, kumbe njia yao ni mzunguko unaoenda kushoto.

You can share this post!

Kimathi aelekea Ureno kupaisha gari duru ya dunia

NJENJE: Pigo kwa wafugaji kuku nchini bei ya mayai ikishuka...

T L