• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
NJENJE: Pigo kwa wafugaji kuku nchini bei ya mayai ikishuka pakubwa

NJENJE: Pigo kwa wafugaji kuku nchini bei ya mayai ikishuka pakubwa

NA WANDERI KAMAU

BEI ya mayai imeshuka kwa asilimia 20 nchini kutokana na ongezeko la uingizaji wake kutoka mataifa ya nje.

Hali hiyo pia imechangiwa na kushuka kwa kiwango cha matumizi ya bidhaa hiyo miongoni mwa Wakenya.

Kwa sasa, kreti moja ya mayai inauzwa kwa Sh360, ikilinganishwa na Sh450 mwezi Aprili.

Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji Kuku Kenya (KPA), Bi Wairimu Kariuki, alisema kuwa kando na ongezeko la uingizaji wa mayai kutoka nchi za nje, wafugaji kuku wana akiba kubwa ya mayai.

Anasema kuwa kiwango hicho kimeongezwa na hali ya kuimarika kwa uchumi, baada ya janga la virusi vya corona.

Uhaba wa mayai miezi miwili iliyopita ulifanya bei yake kupanda sana. Wakulima wengi walilazimika kuanza kuuza kuku kutokana na ongezeko la bei za vyakula vya kuwalisha.

“Wakulima wana akiba kubwa ya mayai kwani kuku walionunua wakati wa msimu wa corona sasa wameanza kutaga,” akaeleza Bi Kariuki.

Akaongeza: “Matumizi yake pia yamepungua sana kutokana na kushuka kwa nguvu ya Shilingi ya Kenya. Vile vile, sekta ya hoteli bado haijaimarika kabisa.”

“Bei ya mayai imeshuka sana kwa kuwa tunapata mayai mengi kutoka Uganda, hali ambayo imeathiri sekta hiyo nchini,” akasema Bw Martin Kinoti, ambaye ndiye Katibu Mkuu wa Chama cha Watengenezaji Vyakula vya Mifugo Kenya (AKNF).

Kupungua kwa bei hiyo kunaonekana kuwa pigo kubwa kwa watengenezaji vyakula vya kuwalishia kuku, kwani wakulima wengi hawavinunui kwa wingi kama ilivyokuwa hapo awali.Kwa sasa, bei ya gunia la kilo 70 la vyakula hivyo ni Sh3,200 kutoka Sh4,000 mwaka 2021.

Kwa muda mrefu, wafugaji kuku nchini wamekuwa wakilalamikia kupungua kwa mapato yao kutokana na ongezeko la mayai kutoka Uganda.

Bei ya juu ya vyakula vya kuku imetajwa kuchangiwa na ongezeko la bei ya mahindi, alizeti na maharagwe aina ya Soya.

You can share this post!

TAHARIRI: Raia atazidi kuumia bila ukomavu wa kisiasa

Uhuru ahimizwa akamnadi Raila Mlima Kenya

T L