• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 5:07 PM
TAHARIRI: Rais, Naibu wake wajue wanachojali wananchi ni huduma pekee

TAHARIRI: Rais, Naibu wake wajue wanachojali wananchi ni huduma pekee

NA MHARIRI

KIPINDI cha siku nne zilizopita kimeshuhudia kwa mara nyingine malumbano kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake William Ruto haswa wakati wa shughuli za mazishi ya aliyekuwa Rais wa Tatu wa taifa, marehemu Mwai Kibaki, na wakati wa sherehe za Leba Dei.

Wakati wa hafla za ibada ya wafu na mazishi ya mwendazake Kibaki, vitendo na maneno kadhaa baina ya viongozi hao wakuu wa nchi vilifasiriwa na wananchi na wachanganuzi kwamba wawili hao bado wamewekeana uhasama mkubwa.

Naibu Rais nyakati zote mbili alinyanyuka akishangiliwa kupitiliza na wafuasi wake, katika ngome ya Rais Kenyatta anayekaribia kuondoka mamlakani.

Usemi wa Dkt Ruto kwamba Rais Kibaki ndiye aliyekuwa rais mzuri zaidi kuwahi kushuhudiwa nchini nao ulichukuliwa na wafuasi wa Bw Kenyatta kama kombora la moja kwa moja kwake lililolenga kumdunisha mbele ya wageni waalikwa.

Kwa upande mwingine, kitendo cha Rais kukosa kumsalimia kwa mkono Naibu wake kilichukuliwa na wafuasi wa Dkt Ruto kwamba ni hatua ya kumdunisha.

Kilele cha vita hivi baridi kikawa Jumapili ambapo Rais alimshambulia Naibu wake kwa kukataa kufanya kazi naye badala yake akiamua “kutangatanga” kwenye masoko akikashifu serikali aliyomo ndani bila kujiuzulu.

Naibu naye akajibu kwa kumkumbusha jinsi ‘alivyomnyang’anya’ majukumu na kuyapa watu fulani akiwemo ‘mzee aliye mradi wake’ (Raila Odinga).

Ama kwa kweli ni majibizano yaliyoacha wengi vinywa wazi ingawa kwa wachanganuzi na waangalizi, ilikuwa hali ambayo haistahili kushuhudiwa kwa vyovyote nchini.

Wananchi walioamka asubuhi na mapema kwenda kupiga kura 2017 walitarajia kwamba viongozi waliochaguliwa watatumia muda wao wote na kwa hali na mali, kutatua matatizo mengi yanayowakumba.

Na matatizo yenyewe hata yamekuja kuongezeka kufuatia janga la corona na kwa sasa hivi makabiliano yanayoendelea baina ya Urusi na Ukraine, kwa hivyo iwapo kuna wakati ambapo wananchi wanategemea serikali yao iwaangalie, ni sasa hivi.

Kwa hakika, hakuna Mkenya yeyote anayejali kuhusu tofauti za kibinafsi baina ya Rais Kenyatta na Naibu wake William Ruto.

Hata wakijua haitawasaidia kwa vyovyote.

Wangwana hawa wawili hawana budi kuvumiliana na kuhudumia Wakenya hadi pale serikali yao itafikia kikomo Agosti 9.

You can share this post!

Vipusa wafuzu tenisi ya Afrika

Man-United wararua Brentford katika EPL uwanjani Old...

T L