• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 5:50 AM
Man-United wararua Brentford katika EPL uwanjani Old Trafford

Man-United wararua Brentford katika EPL uwanjani Old Trafford

Na MASHIRIKA

MANCHESTER United walisajili ushindi mnono zaidi chini ya kocha mshikilizi Ralf Rangnick kwa kupepeta Brentford 3-0 mnamo Jumatatu usiku uwanjani Old Trafford.

Mechi hiyo ilikuwa ya mwisho kwenye kampeni za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kwa miamba hao wa zamani kutandaza katika uwanja wao wa nyumbani msimu huu.

Kiungo mvamizi Bruno Fernandes aliwafungulia Man-United karamu ya mabao katika dakika ya tisa kabla ya Cristiano Ronaldo kufunga penalti katika dakika ya 61 kisha beki Raphael Varane kuzamisha kabisa chombo cha wageni wao kunako dakika ya 72. Goli la Varane lilikuwa lake la kwanza kambini mwa Man-United.

Ronaldo sasa amefikisha mabao 18 kwenye EPL muhula huu na idadi hiyo inamweka katika nafasi ya pili nyuma ya Mohamed Salah wa Liverpool anayeongoza orodha ya wafungaji bora kufikia sasa kwa mabao 22.

Huku ushindi huo wa Man-United ukiweka hai matumaini yao finyu ya kufuzu kwa soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu ujao, Brentford sasa huenda wakajipata wakiteremshwa ngazi kwenye EPL muhula ujao iwapo watashindwa kuhimili presha kutoka kwa Southampton, Burnley, Leeds United na Everton.

Wakisalia na mechi mbili pekee kwenye kipute cha EPL muhula huu, Man-United kwa sasa wanakamata nafasi ya sita jedwalini kwa alama 58, tatu nyuma ya nambari tano Tottenham Hotspur na tano nyuma ya Arsenal wanaofunga orodha ya nne-bora. Hofu zaidi kwa Man-United ni kwamba Arsenal na Spurs wana mechi mbili zaidi za kutandaza ili kufikia idadi ya michuano 36 ambayo wao wamesakata.

Ushindi katika mechi mbili zijazo utashuhudia Man-United wakikamilisha msimu kwa jumla ya pointi 64, hiyo ikiwa idadi sawa ya alama na waliyojizolea mnamo 2013-14 chini ya kocha David Moyes. Idadi ndogo zaidi ya alama ambayo Man-United wamewahi kujivunia katika historia yao kwenye EPL ni pointi 59 mnamo 1990-91.

Matokeo dhidi ya Brentford ndiyo bora zaidi kuwahi kusajiliwa na Man-United msimu huu, na yalichochewa na ubunifu wa kiungo Juan Mata aliyepangwa katika kikosi cha kwanza cha EPL kwa mara ya kwanza katika mechi ambayo huenda ni yake ya mwisho kuchezea Man-United ugani Old Trafford.

Bao la Fernandes ambaye anatarajiwa kuwa nguzo muhimu ya Man-United chini ya kocha mpya Erik ten Hag kuanzia msimu ujao, lilikuwa lake la kwanza tangu Februari 2022. Mkataba wa sasa kati ya Man-United na kiungo huyo raia wa Ureno unatarajiwa kukatika mwaka wa 2026.

Wakitegemea zaidi maarifa ya Ronaldo, Man-United walishuka dimbani wakipania kuendeleza ubabe uliowawezesha kutoka nyuma na kulazimishia Chelsea sare ya 1-1 katika mchuano wa awali wa EPL nyumbani.

Matumaini ya Man-United kutinga nne-bora ligini msimu huu yaliyoonekana kuyeyuka baada ya kupoteza mechi tatu kati ya tano huku wakishinda mchuano mmoja pekee kutokana na sita za awali kabla ya kualika Brentford.

Wanapopigania fursa ya kufuzu kwa soka ya Europa League msimu ujao, wanakabiliwa pia ushindani mkali kutoka kwa West Ham United wanaofunga orodha ya saba-bora kwa pointi 52 baada ya mechi 35. Man-United watafunga kampeni za EPL msimu huu dhidi ya Brighton na Crystal Palace kwa usanjari huo.

Brentford sasa wameshinda mechi 11, kuambulia sare mara saba na kupoteza michuano 17 kati ya 35 iliyopita ambayo imewazolea alama 40 sawa na Aston Villa na Southampton. Walijibwaga ugani wakijivunia kuokota alama 10 kutokana na mechi nne zilizopita za EPL baada ya kushinda Chelsea, West Ham na Watford kabla ya kuambulia sare tasa dhidi ya Tottenham Hotspur.

Brentford sasa wameshinda mechi tano na kupoteza mbili kati ya nane zilizopita. Watakamilisha msimu kwa michuano dhidi ya Southampton, Everton na Leeds United.

Brentford wanaoshiriki EPL kwa mara ya kwanza tangu 1946-47, walipigwa na Man-United 3-1 katika mkondo wa kwanza wa EPL msimu huu mnamo Januari 2022. Mechi dhidi ya Man-United ilikuwa yao ya kwanza kutua Old Trafford tangu Septemba 1975 walipotandikwa 2-0 katika League Cup.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Rais, Naibu wake wajue wanachojali wananchi ni...

Nitaongoza Wakenya kupata uhuru wa kiuchumi – Raila

T L