• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 3:13 PM
TAHARIRI: Ruto, Gachagua waache siasa, ni wakati wa kuchapa kazi

TAHARIRI: Ruto, Gachagua waache siasa, ni wakati wa kuchapa kazi

NA MHARIRI

KAULI za viongozi wakuu wa serikali wanazoendelea kutamka hadharani zinatia Wakenya wasiwasi kuhusu kujitolea kwao kuiendeleza nchi mbele.

Rais William Ruto na naibu wake wameendelea kulaumu viongozi wa upinzani kwa masaibu yanayowakumba Wakenya.

Naibu Rais, Bw Rigathi Gachagua jana Jumapili aliendelea kudai kuwa serikali ilikuta hazina ikiwa haina pesa za kufanyia maendeleo. Kwamba kulikuwa na Sh93 milioni pekee.

Kauli hiyo ilikanushwa na Gavana wa Benki Kuu ya Kenya, aliyesema kawaida katika masuala ya kifedha, punde baada ya bajeti pesa husambazwa kwa wizara na idara husika.

Jana Jumapili wakiwa Kericho, rais na naibu wake waliendelea kuwataka walioshindana nao uchaguzini kuwa wapinzani wao.

Kauli hiyo inaonyesha kuwa serikali bado iko kwenye hali ya kampeni, ilhali zilimalizika Agosti 6.

Jukumu la serikali kwa sasa si kulaumu upinzani, kiangazi au sababu yoyote nyingine.

Walipoomba kura, waliahidi kutatua shida za mwananchi. Shida hizi ni pamoja na gharama ya maisha. Kuna ukosefu wa ajira, kulemaa kwa biashara kati ya mambo mengine.

Matarajio ya wananchi ni kwamba mambo haya yatashughulikiwa kwa haraka.

Wananchi wanatarajia kuambiwa serikali imefikia wapi katika kupunguza bei ya chakula.

Mnamo Ijumaa, bei ya mafuta ilipungua kwa Shilingi moja. Hili ni jambo ambalo serikali ingelitumia kuwaeleza wananchi kwamba angalau imeanza juhudi za kupunguza gharama ya maisha.

Kuwalaumu wapinzani kunaenda kinyume na msimamo wa Rais alipokula kiapo, ambapo alisema angependa kuwe na upinzani wa nguvu.

Alitangaza kwamba hatawapa kazi wapinzani wake, kwa sababu anataka kuwe na uongozi wa upinzani wenye kauli nzito. Ni kupitia kauli za wapinzani ambapo serikali itagundua makosa yake na kuwafanyia kazi wananchi.

Ahadi aliyotoa jana kwamba Hazina ya Mahasla itaanza kuwepo Disemba, ni mojawapo ya hatua nzuri kwa serikali ya Kenya Kwanza. Watu milioni saba waliompigia kura Dkt Ruto, walifanya hivyo kutokana na matumaini makubwa aliyowapa.

Iwapo serikali inahitaji muda wa kujipanga ili kutimiza ahadi hizo, inaweza kuomba muda huo bila ya kuonekana kuwa haina mipango mizuri.

Kulalamika hadharani na kuwekelea lawama watangulizi, huenda isiwe mbinu bora ya kuwatuliza Wakenya. Kauli hizi zinaweza kuchukuliwa kuwa visingizio. Serikali iweke mpango wa kutoa taarifa zake kirasmi angalau mara moja kwa wiki, ambapo itakuwa ikieleza hatua ilizopiga, bila ya kuonekana kama inayoanza kampeni za uchaguzi mkuu wa 2027.

You can share this post!

MWALIMU WA WIKI: Nyimbo na maigizo ni siri yake darasani

Duale asema alinukuliwa visivyo madai kwamba angefichua...

T L