• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 2:19 PM
MWALIMU WA WIKI: Nyimbo na maigizo ni siri yake darasani

MWALIMU WA WIKI: Nyimbo na maigizo ni siri yake darasani

NA CHRIS ADUNGO

KWA kawaida, kusoma na kuandika kunastahili kusisimua na kuchangamsha.

Hata hivyo, kuna uwezekano baadhi ya wanafunzi wawe na mitazamo hasi kuhusu stadi hizi muhimu.

Ikitokea hivyo, mwalimu huwa na jukumu la kufanya vipindi vya somo lake darasani kuwa vya kusisimua. Njia moja ya kuamsha ari ya wanafunzi kuthamini masomo ni kushirikisha nyimbo na michezo ya kuigiza katika shughuli za ufundishaji.

Haya ni kwa mujibu wa Bw Franklin Mukembu ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Idara ya Kiswahili katika shule ya Munithu iliyoko Imenti Kaskazini, Kaunti ya Meru.

“Nyimbo na maigizo hufanya wanafunzi waelewe mambo haraka na huwaamshia hamu ya kujifunza vitu vipya. Huchochea ubunifu miongoni mwao na huwapa majukwaa mwafaka ya kutambua, kukuza na kulea vipaji vyao,” anasema.

Mukembu alizaliwa katika kata ya Kajuki, eneobunge la Chuka-Igambang’ombe, Kaunti ya Tharaka-Nithi. Alianza safari ya elimu katika shule ya msingi ya Kithinge, Kajuki (1988-1996) kabla ya kujiunga na shule ya upili ya Chogoria Boys, Chuka (1997-2000).

Alisomea ualimu (Kiswahili/Jiografia) katika Chuo Kikuu cha Egerton kati ya 2002 na 2006.

Aliwahi kufundisha katika shule ya Kiriani iliyoko Maara, Tharaka-Nithi (2006-2008) kabla ya Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC) kumwajiri mwaka wa 2008 na kumtuma katika shule ya Munithu.

Haja ya kujiendeleza kitaaluma ilimpa msukumo wa kujiunga na Chuo Kikuu cha Kenyatta mnamo 2012 kusomea shahada ya uzamili.

Alifuzu 2016 baada ya kuwasilisha tasnifu kuhusu ‘Sayansi bunilizi katika riwaya teule’ chini ya usimamizi na uelekezi wa Prof Kitula King’ei na Dkt Richard Wafula.

Mukembu amekuwa mtahini wa insha za Kiswahili katika Baraza la Kitaifa la Mitihani (KNEC) tangu 2016.

Tajriba anayojivunia katika ufundishaji na utahini imempa fursa tele za kuzuru shule mbalimbali za humu nchini kwa nia ya kuhamasisha, kushauri na kuelekeza walimu na wanafunzi kuhusu mbinu mwafaka za kujiandaa kwa mitihani ya kitaifa.

Zaidi ya ualimu, Mukembu pia ni mshairi shupavu na mchangiaji wa makala, tahakiki na maoni katika magazeti ya ‘Taifa Leo’ na ‘Daily Nation’.

Anajivunia kuchapishiwa vitabu ‘Ruwaza ya Insha’ na ‘Mwongozo wa Tamthilia ya Bembea Ya Maisha’ (Timothy Arege).

‘Financial Implications and Solutions’ na ‘Literary Insights and Jargon’ ni baadhi ya kazi zake ambazo sasa ziko katika hatua za mwisho mwisho za uhariri katika kampuni na mashirika mbalimbali ya uchapishaji wa vitabu humu nchini.

Mukembu amekuwa akishirikisha wanafunzi wake katika mashindano ya uandishi ya Digital Essay (DEC) yanayoendeshwa na eKitabu.

Mnamo 2018, mwanafunzi wake aliambulia nafasi ya tatu na kujizolea rununu na kitita cha Sh10,000 katika kitengo cha Insha za Kiswahili.

Mwanafunzi wake mwingine alituzwa rununu na Sh50,000 mnamo 2020 baada ya kuibuka wa kwanza nchini Kenya.

Mbali na kuwa miongoni mwa waamuzi wa DEC, Mukembu pia ni mtunzi na mwelekezi stadi wa michezo ya kuigiza katika mashindano ya shule, makanisa na mashirika.

Isitoshe, amekuwa mwamuzi wa kiwango cha kaunti katika tamasha za kitaifa za muziki na drama tangu 2016. Aliwahi kuwa mwendeshaji wa kipindi ‘Chemchemi ya Lugha’ katika Radio Tuliza 92.4 FM mnamo 2020.

  • Tags

You can share this post!

Ebola: Uganda sasa yaweka ‘lockdown’

TAHARIRI: Ruto, Gachagua waache siasa, ni wakati wa kuchapa...

T L