• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
TAHARIRI: Sekta kuu za kilimo zifufuliwe

TAHARIRI: Sekta kuu za kilimo zifufuliwe

NA MHARIRI

MANIFESTO ya muungano wa Kenya Kwanza wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu uliopita ilivutia Wakenya wengi hasa kutokana na azimio moja; kuvumisha sekta ya kilimo ambayo inaendelea kuanguka.

Rais William Ruto kwenye ahadi yake kuhusu kilimo alikariri mpango wake wa kurejesha umaarufu na utukufu wa kilimo cha miwa, pamba, majani-chai na kahawa, ambacho hapo awali kilizipa riziki familia nyingi sana nchini.

Kuanguka kwa viwanda vya sukari vya Mumias, Miwani, Nzoia, Sony, Ramisi na vinginevyo kuliwazulia watu wengi mahangaiko makubwa.

Wengi walishindwa kulisha familia zao, wakashindwa kuwalipia watoto wao karo, wakazidiwa na gharama za matibabu na hivyo basi kuchangia wengi kuenda jongomeo mapema.

Hali ni hiyo hiyo kwa wakulima waliotegemea pamba, pareto, majani-chai na kahawa.

Hata ingawa kwa kiwango fulani ukuzaji wa majani-chai na kahawa bado unaendelea, kudorora kwa sekta hizo za kilimo kuliibua matatizo sawa na yale yanayoshuhudiwa na wakuzaji miwa.

Japo Rais Ruto ameanza kwa kukabiliana na changamoto zinazokumba kilimo cha mahindi, kama vile kupunguza bei ya mbolea, hajaonyesha bayana jinsi atakavyofufua kilimo cha miwa.

Aidha, Rais anastahili hongera kwa kuonyesha nia ya kukirejeshea uhai kilimo cha kahawa na majani-chai, baada ya kumpa naibu wake, Bw Rigathi Gachagua, jukumu la kuongoza juhudi za kutatua shida zinazokumba sekta hizo mbili.

Ni muhimu Dkt Ruto afahamu kwamba wakuzaji miwa hasa katika eneo la magharibi mwa Kenya wangali wanasubiri kwa matumaini mipango ya kuhuisha kilimo cha miwa.

Hata ingawa huenda wapo makabaila wanaotamani sana sekta hizi ziendelee kufifia ndipo wapate mwanya wa kuagiza bidhaa hizo kutoka nje ya nchi kwa manufaa yao ya kibinafsi, serikali ya Kenya Kwanza inafaa itumie mabavu kuwazima ili kuwanusuru raia wasiokuwa na usemi wowote.

Ufufuzi wa sekta hii, vilevile, utasaidia nchi hii kupunguza tatizo la ukosefu wa kazi. Mamilioni ya vijana wa Kenya wenye ujuzi na utaalamu unaohitajika ili kuinua uchumi wamekuwa ‘wakipiga lami’ na vyeti vyao bila mafanikio.

Iwapo kilimo cha miwa, pamba, kahawa na majani-chai kitapewa umuhimu jinsi Kenya Kwanza ilivyoahidi, wengi wa vijana hawa waliofuzu na hata wasioelimika sana, watapata nafasi za ajira.

Kwa mfano, kilimo cha pamba kitachangia kuanzishwa kwa viwanda vya kutengeneza nguo ambavyo vitawapa maelfu ya vijana nafasi za kazi. Ingawa sekta ya teknolojia na dijitali imeunda nafasi nyingi za kazi, bado pana haja ya kuimarisha kilimo ambacho bado ndicho uti wa mgongo wa uchumi wa nchi hii.

Tunaitia shime serikali ya Dkt Ruto kuharakisha mikakati ya kutimiza ahadi ya ukuzaji kilimo.

  • Tags

You can share this post!

LISHE: Faida na manufaa ya mafuta ya kanola

WANDERI KAMAU: Licha ya misukosuko Afrika ni bara lenye...

T L