• Nairobi
  • Last Updated December 5th, 2023 10:25 PM
WANDERI KAMAU: Licha ya misukosuko Afrika ni bara lenye baraka tele!

WANDERI KAMAU: Licha ya misukosuko Afrika ni bara lenye baraka tele!

NA WANDERI KAMAU

AFRIKA imebarikiwa. Kwa muda mrefu, Afrika imekuwa mfano wa bara lililotengwa duniani.

Bara la mateso, mahangaiko, vilio, njaa, vita na uhasama baina ya mtu na ndugu yake, jamii baina ya jamii na nchi baina ya nchi.

Dhana hizo ziliendelezwa na kufikia upeo kiasi kwamba, wanahistoria waliibandika Afrika kuwa ‘Bara la Giza’ (Dark Continent).

Vitabu vya historia vilivyoandikwa na wasomi kutoka Ulaya, viliisawiri Afrika kama bara la watu waliokaribiana na nyani kimaumbile.

Hicho ndicho kiwango ambacho Afrika na Waafrika walikuwa wamechukuliwa na Wazungu.

Kinaya ni kuwa, licha ya dhana hizo zote Afrika bado imeendelea kuwa bara la kipekee. Bara ambalo limebarikiwa kwa kila namna.

Kwanza, ni nadra Afrika kushuhudia mitetemeko ya ardhi; kama lililotokea katika nchi za Uturuki na Syria, ambapo kufikia sasa zaidi ya watu 19,000 wamefariki.

Kijiografia, Afrika iko mahali ambapo ni vigumu sana kukumbwa na mitetemeko kama hiyo.

Tunawapa pole waathiriwa wote wa janga hilo.

Ukweli ni kuwa kwa kutokumbwa na mikasa kama hiyo ya kimazingira, hii ni baraka ambayo Waafrika wanafaa kujivunia .
Pili, Afrika haishuhudii misimu mikali ya baridi au kiangazi, bali misimu yake huwa ya kadri.

Wakati wa msimu wa baridi katika mataifa ya bara Ulaya, wenyeji hulazimika kutumia umeme ili kuweka joto nyumba zao.
Wengine hata hununua mashine za kuipa miili yao joto!

Zaidi ya hayo, baadhi hulazimika kutotoka nje ili kujikinga na baridi kali ya barafu ambayo hukumba mataifa hayo.
Barani Afrika, hali ni tofauti kabisa. Msimu wa baridi huwa kadri.

Kinaya ni kuwa, Wazungu huja barani humu kupata joto la jua wakati baridi imetanda nchi zao.

Tatu, ingawa wakati mwingine Afrika hukumbwa na kiangazi cha muda mrefu, kiwango cha joto huwa cha kadri.

Ni vigumu kusikia Waafrika wakipatwa na matatizo ya ngozi kutokana na makali ya joto la jua.

Katika baadhi ya mataifa ya Ulaya, Amerika, Asia na Mashariki ya Kati, simulizi hizi ni kawaida.

Si mara moja tumesikia visa vya watu kupata maradhi ya ngozi, kama vile saratani, kwa sababu ya athari za joto kali. Haya hayajawahi kusikika Afrika.

Ingawa hatusemi Afrika haina matatizo yake, ukweli ni kuwa kinyume na dhana ambayo imekuwa ikiendelezwa na kuenezwa kwa muda mrefu, Afrika ni bara lililobarikiwa sana.

Kando na majanga kama mitetemeko ya ardhi, ni vigumu pia kusikia matukio kama dhoruba au vibunga—hata katika nchi zilizo na ufuo wa bahari kama Kenya, Tanzania au Msumbiji.

Ikiwa majanga hayo hutokea, huwa nadra sana.

Waafrika tujivunie kuwa bara hili ni kati ya maeneo bora zaidi pa kuishi duniani kwa sasa.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Sekta kuu za kilimo zifufuliwe

CECIL ODONGO: Viongozi wa ODM walioenda Ikulu ni wasaliti,...

T L