• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 1:14 PM
TAHARIRI: Serikali, Azimio wajue hatima ya nchi ni kwao

TAHARIRI: Serikali, Azimio wajue hatima ya nchi ni kwao

NA MHARIRI

MATUMAINI yote ya Wakenya yatakuwa kwa kamati zinazoiwakilisha mirengo ya Kenya Kwanza na Azimio la Umoja kwenye Mazungumzo ya Maridhiano yatakayoanza leo katika Ukumbi wa Bomas, jijini Nairobi.

Mrengo wa Kenya Kwanza unawakilishwa Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Kimani Ichung’wa (anayewaongoza), Kiongozi wa Wengi katika Seneti Aaron Cheruiyot, wabunge Hassan Omar (Bunge la Afrika Mashariki-EALA), Catherine Wambilianga (Bungoma) na Gavana Cecily Mbarire (Embu).

Mrengo wa Azimio, kwa upande wake, unawakilishwa na Kiongozi wa Wiper- Kalonzo Musyoka (kiongozi wa ujumbe), Kiongozi wa Wachache Opiyo Wandayi, Seneta Okong’o Omogeni (Nyamira), mbunge Amina Mnyazi (Malindi) na aliyekuwa Waziri wa Ulinzi, Eugene Wamalwa.

Bila shaka, watu hao 10 ndio tegemeo kuu la Wakenya kusuluhisha mivutano ambayo imekuwepo baina ya Rais William Ruto na Kiongozi wa Azimio, Bw Raila Odinga.

Wanapoanza kuweka mikakati ya kujadili masuala tata ambayo yameibuliwa na kila mrengo, wito wetu kwao ni kushusha misimamo yao mikali, na kukumbuka kuwa wamebeba na kuwakilisha mustakabali wa kiuchumi na kisiasa wa zaidi ya Wakenya milioni 50.

Tunawarai viongozi hao kushiriki kwenye mazungumzo hayo kama vile wachezaji wa kandanda huwa wanashiriki kwenye mchezo huo.

Katika kandanda, huwa kuna refa, ambaye ndiye huwa mwamuzi mkuu kuhusu mwelekeo ambao mchezo husika utachukua.

Pia, mchezo huo huwa unadhibitiwa sheria, ambazo lazima ziheshimiwe na kuzingatiwa na kila mchezaji.

Wakati refa anapomwadhibu mchezaji, kwa mfano, kwa kumpa kadi nyekundu ama kadi ya manjano, mchezaji husika huwa anatii maagizo ya refarii, bila kumkaidi.

Katika mazingira kama hayo, mchezo huwa unaendelea na kukamilika bila matatizo yoyote kuibuka. Washiriki wote huheshimu matokeo ya mchezo: wanaoshinda na wanaoshindwa.

Vivyo hivyo, tunawarai viongozi hao kuwa na mtazamo huo, wanapoingia katika ukumbi wa Bomas. Waheshimu ‘refa’ Obasanjo.

Pili, tunawarai kuheshimu maagizo yatakayowekwa ili kudhibiti mchakato huo.

Tatu, wito wetu kwao ni kuheshimu maamuzi ya mwisho ya mchakato huo. Ikiwa watazingatia hayo, watakuwa wamewafanyia haki Wakenya wote wanaowatazama na kutegemea maamuzi yao kutoa mwelekeo wa mwisho wa nchi.

Ni lazima waweke ubinafsi pembeni Ni muhimu wakumbuke madhara ya mapigano yaliyotokea nchini baada ya uchaguzi tata wa 2007, ambapo zaidi ya Wakenya 1,300 walifariki huku wengine zaidi ya 600,000 wakiachwa bila makao.

Ni wakati mwafaka kwa viongozi hao kumi kuiokoa Kenya na kuifungulia ukurasa mpya wa utulivu, utangamano na maridhiano.

  • Tags

You can share this post!

Mapenzi jamani! Huyu unayempenda anampenda yule

Koome ahamisha jaji aliyepiga breki Sheria ya Fedha ya 2023

T L