• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 9:01 PM
TAHARIRI: Serikali inayoingia isipuuze matatizo ya afya ya akili yanayokumba raia

TAHARIRI: Serikali inayoingia isipuuze matatizo ya afya ya akili yanayokumba raia

NA MHARIRI

MOJAWAPO ya mambo muhimu ambayo serikali mpya inapaswa kuayaangazia kwa haraka ni afya ya akili.

Sekta ya afya imegatuliwa lakini afya ya akili ni jambo ambalo serikali ya kitaifa haina budi kulishughulikia, ikiwa itahitaji kufanikiwa kwenye utekelezaji wa sera zake za kiuchumi na kijamii kwa jumla.

Kati ya watu walioathiriwa zaidi na tatizo hili ni maafisa wa usalama. Kisa cha Jumatatu ambapo afisa wa polisi wa cheo cha Maoni OCS kituo cha polisi cha Mau Summit aliua mpenzi wake kisha akajiua.

Mwanzoni mwa mwaka huu, mtaalamu wa masuala ya akili, Dkt Frank Njenga, alihusishwa katika mazungumzo ya kuangalia chanzo cha maafisa hao kujihusisha katika mauaji.

Kama Dkt Njenga alitoa ripoti, yafaa ishughulikiwe na mapendekezo yake yatekelezwe. Iwapo hajatoa ripoti, maafisa watakaoingia afisini anapaswa kuanza kufuatilia suala hilo na kujua yaliyojadiliwa. Wajaribu kuelewa masuala makuu yanayowafanya polisi kuwa wepesi wa kuua au kujiua.

Baada ya hayo, serikali pia ifuatilie kinachofanya wananchi kuuana au kujiua baada ya migogoro. Kuna ongezeko la visa vya watu kujiua au kuua wengine kutokana na mizozo ya kinyumbani, kutoelewana kuhusu ugavi wa mali, urithi wa mashamba au watu kudaiana na kudaiwa.

Ni mwezi Agosti tu ambapo mwanaume alichoma nyumba na kujaribu kujiua katika Kaunti ya Kisii kwa kulemewa na mkopo aliokuwa amechukua kutoka kwa chama cha ushirika.

Vijana pia wamekuwa wakijiua au kuua wazazi wao kwa kudai kugawiwa mashamba au kuonyesha mahali pa kulima. haya yote yanaashiria kuwa tatizo kubwa zaidi ni uchumi.

Mamilioni ya Wakenya walioidhinisha chaa cha UDA na muungano wa Kenya Kwanza kwa jumla kuingia uongozini, walishawishiwa na matumaini waliyopewa wakati wa kampeni.

Wengi wao waliahidiwa kutolewa kutoka kwa CRB, wakiwa wamelemewa na mikopo waliyochukua.

Tayari Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru (KRA) imetangaza kwamba kuanzia Oktoba 1, bei za bidhaa muhimu zitapanda kutokana na kupanda kwa ushuru kwa asilimia sita.

Hiyo ina maana kwamba bila shaka bei za bidhaa muhimu zitakuwa ghali zaidi ya ilivyo sasa. Mojawapo ya ahadi kuhusiana na suala hili ni kupunguza gharama ya maisha. Hali ya watu kutoweza kutimiza mahitaji ya lazima, hasa chakula, huenda ikawa sababu kuu ya ongezeko la msongo wa mawazo.

Serikali pia inaweza kuanzisha somo katika mtaala wa elimu, watu wafunzwe jinsi ya kukabiliana na changamoto. Ilivyo kwa sasa, ni wazi kuwa vijana wengi hawajafunzwa kwamba maisha yana kupanda na kushuka.

  • Tags

You can share this post!

Kylian Mbappe aongoza PSG kuzamisha chombo cha Juventus...

JURGEN NAMBEKA: Rais mteule atekeleze ahadi zake kwa...

T L