• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 5:50 PM
TAHARIRI: Serikali iweke sera za kudhibiti kupandisha nauli

TAHARIRI: Serikali iweke sera za kudhibiti kupandisha nauli

KITENGO  cha UHARIRI

RIPOTI ya utafiti wa shirika la Infotrak inaonyesha zaidi ya nusu ya Wakenya watasherehekea Sikukuu ya Krismasi wakiwa hawana namna.

Kwamba ingawa huu ni msimu wa watu kujumuika na jamaa zao kusheherehekea, gharama ya juu ya maisha imewazuia kusafiri mashambani.Kutokana na ugumu huo wa maisha, watu wengi wameamua kuwa si lazima kusafiri kwenda kwao wakati huu. Lakini si wote walio na hiyari.

Kuna wanafunzi waliofunga shule na wanatakikana kusafiri na kujiunga na wazazi wao katika pembe mbalimbali za nchi.Kwa hivyo wanahitaji usafiri salama na rahisi wa kuwafikishwa kwao. Serikali imejaribu kwa kiwango kikubwa kuweka usafiri mzuri kupitia shirika la Reli.

Kuna garimoshi ya kusafiri kati ya Mombasa na Nairobi (SGR) na lile la kati ya Kisumu na Nairobi.Ingawa huduma za garimoshi la Kisumu na Nairobi hazijaboreka vile, hiyo ni hatua nzuri katika kuimarisha uchukuzi. Jumanne usiku abiria walikesha barabarani baada ya taarifa za Kenya Railways kusema garimosho lilikwama katika eneo moja kabla ya kufika Kisumu.

Mbali na tukio hilo moja, uchukuzi huo wa garimoshi ungekuwa bora kama serikali ingetafuta mbinu za kufanya liende kwa kasi kama lile la SGR.Mtu kusafiri chini ya kilomita 400 kwa zaidi ya saa 12 si haki. Kweli nauli ya garimoshi ni rahisi, lakini kuna watu wengi wanaopendelea kutumia muda mchache kufika wanakotaka.

Ndio sababu wamiliki wa matatu na mabasi wameamua kuwanyonga abiria wanaotafuta usafiri. Kwa sasa, watu wanaoenda mashambani wamepandishiwa nauli, hata mara mbili ya ile ya kawaida. Kwa mfano, japokuwa kusafiri kati ya Nairobi na Eldoret haizidi Sh1,000, hivi sasa baadhi ya matatu zinalipisha hata Sh3,500.

Hali hii inatarajiwa kuwa mbaya zaidi kuanzia kesho, ambapo wale waliokuwa hawajafunga kazi, watakuwa wanawahi mashambani.Huu ni upunjaji ambao yafaa ukomeshwe. Wakati wa Rais Mstaafu Mwai Kibaki, serikali ilitangaza kuwa soko ni huru. Kila mtu ana uamuzi wa kuuza bei aitakayo.

Wenye matatu wakiwa wafanyibiashara, wana uhuru wa kutoza nauli watakayo. Lakini sharti kuwe na sababu za msingi za kufanya hivyo. Kama safari huwa Sh1,000, ni kipi kinachofanya sasa iwe Sh3,500?Hata kama ni kuzingatia kanuni ya biashara kuwa kadri mahitaji ya abiria yanavyoongezeka, kunakuwa na uchache wa magari, nauli haifai kupanda kwa kiwango cha juu.

Kuruhusu watu wa matatu walipishe zaidi ya mara tatu ya nauli ya kawaida, ni kuonyesha kutojali.Serikali yapaswa kuunda sera ambazo zitahakikisha hata abiria wanaotumia matatu na mabasi hawatozwi nauli inayopita asilimia 50. Hayo yawekwe kwenye sheria iliyounda vyama vya ushirika vya magari ya uchukuzi na utekelezaji wake ufuatiliwe kwa karibu.

You can share this post!

4 waaga ajali zikiendelea kuongezeka

Serikali za Uganda, Kenya zakubaliana kusitisha sheria tata...

T L