• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 8:55 PM
TAHARIRI: Sote tuwe washindi katika kura juma lijalo

TAHARIRI: Sote tuwe washindi katika kura juma lijalo

NA MHARIRI

HARAKATI ya maandalizi ya uchaguzi mkuu uliosubiriwa kwa hamu na ghamu imekamilika.

Kampeni zote zinaisha kesho Jumamosi kisheria.

Lakini kama desturi, lazima wananchi wana dukuduku kuu mioyoni mwao wakiwaza matokeo yatakavyokuwa baada ya uchaguzi huo wa Jumanne ijayo.

Kinyang’anyiro kinachozua hofu kwa wengi ni cha urais ambapo kila mtu anaomba, kutamani na kutumai mwaniaji wake wa urais atashinda.

Vivyo hivyo, japo kwa kiwango kidogo, hali ya wahaka inawatatiza raia wengi kuhusu ni mwaniaji yupi wa ugavana, useneta, ubunge na udiwani atakayeibuka mshindi.

Muhimu kwa sasa ni kumtakia kila la heri, lakini muhimu zaidi, ni kujiandaa kukubali matokeo yatakayotangazwa hasa iwapo kura hizo zitakuwa huru na za haki.

Mawazoni twafaa tufahamu kuwa mustakabali wetu umo mikononi mwa Mola wala si katika kiongozi fulani.

Naam, viongozi tunaowachagua huwa na athari katika maisha yetu kutokana na mtindo wao wa uongozi au sera zao, lakini mja hawezi kufahamu kwa uhakika sera za mwaniaji yupi ndizo zitakazomnufaisha zaidi.

Hata hivyo, kunavyo vigezo ambavyo sote twafaa kufuata ili kuwapata viongozi bora juma lijalo.

Sifa za kibinafsi, manifesto na uzoefu wa mwaniaji ni kati ya vigezo vikuu tunavyofaa kuvitumia katika kuwateua viongozi wetu juma lijalo.

Hii ina maana kuwa kiongozi asichaguliwe tu eti kwa sababu ni wa kabila fulani au kutoka na matusi yake dhidi ya mpinzani wake. La hasha hivyo si vigezo bora.

Katika nchi inayostawi kama Kenya, baadhi ya vigezo muhimu ni uadilifu wa mwaniaji, mwaniaji anayehubiri umoja wa kitaifa, maazimio ya ustawi na ufufuzi wa uchumi.

Lakini ipo hali ambapo utamkuta kiongozi asiyedhihirisha sifa hizi akichaguliwa. Hiyo ni demokrasia. Kwa sababu demokrasia inashadidia falsafa ya walio wengi wape, ikifanyika hivyo, basi wewe kama mtu binafsi huna la ziada ila kukubali na kuzingatia jinsi ya kujikuza wewe mwenyewe kibinafsi na familia yako.

Pale ambapo malalamishi yatatokea hasa kuhusu wizi wa kura au mbinu mbovu za uchaguzi, mwathiriwa anahimizwa aelekee mahakamani kutafuta haki.

Hii itatuepushia migogoro hasa ya kikabila kama ilivyoshuhudiwa baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2007.

Maadamu asiyekubali kushindwa si mshindani, sote tuwe tayari kukubali matokeo yatakayopatikana.

You can share this post!

Okutoyi asalimu amri robo-fainali ya wachezaji wawili...

Wazee wakemea wanasiasa kwa kuvuruga Mumias

T L