• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 10:55 AM
TAHARIRI: Tutahadhari sana na aina hii mpya ya corona

TAHARIRI: Tutahadhari sana na aina hii mpya ya corona

Na MHARIRI

WAZIRI wa Afya Mutahi Kagwe juzi alithibitisha kuwepo kwa aina ya Omicron ya Covid-19 nchini Kenya.

Wagonjwa watatu, Wakenya wawili na mmoja kutoka Afrika Kusini walipatikana na aina hiyo na kuwekwa kwenye karantini.

Mutahi alisema atatoa ripoti ya kina baada ya siku mbili ambapo vipimo mbalimbali vitafanywa.

Aina ya Omicron iligunduliwa kwa mara ya kwanza nchini Afrika Kusini mnamo Novemba lakini imeenea sehemu mbalimbali duniani.

Hakika, lilikuwa ni suala la muda tu kabla ya aina hii ya corona ambayo inasifika kuenea kwa kasi sana na kuvuka mipaka yetu.

Takriban wiki mbili zilizopita, Wakenya wengi walipumzika wakati kiwango cha maambukizi ya Covid-19 nchini kilipungua chini ya asilimia moja.

Ndani ya wiki moja, hata hivyo, kiwango cha maambukizi kimepanda hadi asilimia 11.5, juu ya asilimia tano ambayo Shirika la Afya Ulimwenguni linachukulia kuwa ni salama.

Hata hivyo, kuna haja ya kuwa na tahadhari zaidi miongoni mwa Wakenya ili kuepuka kurejea katika ‘lockdown’ ili kudhibiti kuenea kwa virusi hivi vinavyonyumbuka haraka.

Kwetu sisi hapa Kenya, ujio wa virusi vipya unatishia kuweka nchi katika hatari zaidi wakati ambapo nchi inajiandaa kwa uchaguzi mkuu wa 2022.

Shughuli za kisiasa huenda zikaimarishwa katika kipindi hiki, lakini ni sharti tupunguze mijumuiko ya kampeni ikiwa tunataka kukabili Omicron kikamilifu.

Wanasiasa wanaozunguka nchi nzima kwa sasa kutafuta uungwaji mkono wa kisiasa wanapaswa kujidhibiti sasa. Wanahitaji Wakenya wenye afya nzuri kuwapigia kura wakati ukifika.

Kwa vyovyote vile, kuna muda kabla ya kipindi rasmi cha kampeni kutangazwa kuwa wazi na IEBC.

Hivyo basi, ni lazima tuendelee kuzingatia sherehe za kudhibiti corona kama vile kuvaa barakoa, kunawa mikono, kukaa umbali wa mita moja na hata kuchukua chanjo za Covid-19 zinazopatikana katika hospitali za umma kote nchini.

Wakenya hawawezi kupuuza kanuni za afya zilizowekwa na serikali kisha kugeuka kulaani serikali hiyo hiyo wanapolemewa.

You can share this post!

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Baraka zinazoletwa na mazoea ya...

Oparanya apanga kuachia serikali kuu ujenzi wa hospitali ya...

T L