• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 7:53 PM
TAHARIRI: Tutahadhari tukikumbatia vyakula hivi vya GMO

TAHARIRI: Tutahadhari tukikumbatia vyakula hivi vya GMO

NA MHARIRI

MNAMO Jumatatu, Rais William Ruto aliondoa marufuku iliyowekewa vyakula vilivyofanyiwa mabadiliko ya kisayansi almaarufu GMO.

GMO ni ufupisho wa Kimombo wa Genetical Modified Organisms yaani Viumbe Vilivyofanyiwa Mabadiliko ya kisayansi.

Vyakula vilivyofanyiwa utaalamu huo vinahofisha watu wengi kutokana na wasiwasi kuwa huenda mabadiliko hayo yakazua matatizo fulani kwa walaji wa vyakula vya sampuli hiyo.

Mataifa mengi duniani, hasa barani Afrika, yamekuwa yakisita na kuchelea kukumbatia vyakula vya nui hiyo.

Lakini uhalisia ni kuwa vyakula vya aina hii vina mazuri na mabaya yake. Mazuri yake hasa ni kwa sababu, dunia inapoendelea kujaa wanadamu huku sehemu za kukuza mimea zikipungua, hitaji la chakula cha haraka na kinachohimili hali ngumu ya hewa kinahitajika ili kukidhi mahitaji ya watu hawa wengi.

Kwa sasa, kwa mfano, nchini Kenya, ukanda wa Kaskazini Mashariki umeathirika pakubwa na kiangazi, hali ambayo imedidimiza kilimo na kuua mifugo na hata watu.

Hali ni iyo hiyo nchini Somalia na Ethiopia. Watu wanakufa kutokana na njaa iliyosababishwa na kiangazi.

Katika hali kama hii basi, ni bora watu wanaoteswa na njaa wapewe chakula cha GMO wale kuliko kuachwa wafe na njaa.

Vyakula vya GMO vitakuwa na umuhimu mkubwa katika siku zijazo kutokana na ukweli kwamba dunia inazidi kujaa binadamu na hata wanyama ilhali mahali pa kukuza mimea panaendelea kupungua.

Kwa hivyo, ni hekima kwa teknolojia hii, inayoweza kuifanya mimea kukua kwa haraka na katika sehemu ndogo kuzalisha mavuno mengi, ianze kukubaliwa, japo kwa uangalifu mkuu.

Kenya inapokumbatia vyakula vya aina hii, ni muhimu kuwa na tahadhari kubwa maadamu kuna uwezekano wa mabadiliko hayo ya viume kisayansi yakaathiri watumiaji wa chakula cha aina hiyo.

Duniani kunazo juhudi nyingi kwa sasa zinazopigia debe kilimo asilia kisichotumia kemikali zozote kama vile mbolea ya kisasa na hata matumizi ya viuatilifu, yaani dawa za kuwaua wadudu waharibifu.

Juhudi hizo zimebaini kuwa baadhi ya kemikali zinazotoka kwenye pembejeo hizo huingia kwenye mavuno kisha watu wakazila na kuathirika; yamkini ndiyo maana kuna visa vingi vya ugonjwa wa saratani na mengineyo.

Yupo mchangiaji mmoja kwenye mtandao wa kijamii aliyetaka chakula hicho kitiwe lebo inayoonyesha kuwa ni cha GMO. Tunamuunga mkono.

You can share this post!

Club Bruges yakomoa Atletico na kutia guu moja ndani ya...

Mung’aro ateua serikali yake tayari kuanza kazi

T L