• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
TAHARIRI: Uamuzi wa seneti ni funzo kwa magavana, madiwani

TAHARIRI: Uamuzi wa seneti ni funzo kwa magavana, madiwani

NA MHARIRI

HATUA ya seneti kumuondolea Gavana wa Meru lawama alizolimbikiziwa na madiwani inafaa kuwa funzo kwa wawakilishi wa wadi na magavana.

Madiwani wanapaswa kujifunza kwamba hawawezi kumuondoa gavana madarakani bila ushahidi wa kutosha. Pia, inafaa kuwa funzo kwa magavana kuwa wanapigwa darubini katika utendakazi wao, na hivyo basi wanafaa kuwajibika kikamilifu na kufanya kazi yao kwa misingi ya sheria.

Kufanya hivi, na kufuata utaratibu na mchakato wa sheria katika kila hatua na tangazo wanalotoa, kutawahakikishia kinga katika seneti madiwani walio na nia mbaya wakijaribu kuwaondoa mamlakani bila ushahidi wa kutosha.

Hatua ya seneti pia inahakikisha kuwa shughuli katika kaunti hazivurugwi na kwamba madiwani wanapaswa kuepuka mizozo isiyo na maana na wakuu wa kaunti.

Hata hivyo, hii haimaanishi kuwa magavana wanapaswa kuwa vichwa ngumu na kudharau madiwani bali kila upande unapaswa kutekeleza majukumu yake bila kuwa na kinyongo na mwingine.

Uhusiano mzuri, kila upande ukizingatia na kuheshimu sheria, utakuza ugatuzi na kuhakikishia wakazi maendeleo katika maeneo yao. Mizozo ya kila mara kati ya madiwani na magavana imekuwa ikiathiri raia na sio viongozi hao huku wawakilishi wa kaunti wakihujumu ajenda ya kisheria na maendeleo ya wakuu wa kaunti.

Katika demokrasia, tofauti za maoni kati ya viongozi huwa ni jambo la kawaida lakini hazifai kuzua uhasama kiasi cha kuhujumu maendeleo yanayolenga kufaidi wapigakura.

Magavana hawafai kukubali matakwa ya madiwani yaliyo kinyume sheria ili kupata kinga kutoka kwao. Kufanya hivyo ni kuonyesha wako na hatia na wanafahamu hawawezi kutoboa katika seneti madiwani hao wakipitisha mswada wa kuwatimua ofisini.

Hivyo basi, cha msingi ni kudumisha uadilifu wa kikazi na kuheshimu sheria. Mambo haya mawili ni kinga tosha dhidi ya hujuma zozote kutoka kwa yeyote mwenye nia mbaya.

Funzo lingine kwa madiwani ni kwamba hawafai kumezea mate pesa za kaunti na kutumia vitisho kuzipata ilhali wanapaswa kuzilinda dhidi ya kutumiwa vibaya na magavana na serikali zao.

Maseneta katika kutekeleza jukumu lao wako na haki ya kulinda ugatuzi kwa kila aina ya hujuma, ikiwemo kutoka kwa magavana na madiwani wanaoutatiza kupitia vitendo vilivyo kinyume cha sheria.

Kwa kufanya hivyo Wakenya watafurahia matunda ya ugatuzi. Ni makossa kwa watu waliowachagua kuwaongoza kuanza kuzozana. 

  • Tags

You can share this post!

WANDERI KAMAU: Tukome kumlaumu shetani kwa kutojali na...

Jinsi ya kusafisha na kuzuia vinyweleo kuziba

T L