• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 8:55 PM
TAHARIRI: Uhaba huu wa vyakula ni fedheha kwa Kenya

TAHARIRI: Uhaba huu wa vyakula ni fedheha kwa Kenya

NA MHARIRI

IMEKUWA kama desturi kwa Kenya kushuhudia uhaba wa bidhaa za vyakula, ambao punde baadaye hufuatwa na kuagiza shehena kubwakubwa za vyakula kutoka nchi za kigeni.

Tangu jadi, wananchi wa Kenya wamekuwa wakiahidiwa mambo mengi ambayo husemekana yamenuiwa kuboresha uzalishaji wa chakula cha kutosheleza mahitaji ya umma.

Katika miaka michache iliyopita, tuliona jinsi mabilioni ya pesa yalivyowekezwa katika miradi aina hii ikiwemo ya unyunyizaji maji mashambani na ujenzi wa mabwawa yaliyonuiwa kusambaza maji mashambani.

Inasikitisha kuwa tunapoelekea katika uchaguzi mwingine siku chache zijazo, raia bado wanaenda kupiga kura kwa matumaini ya kutatuliwa ahadi zile zile za tangu jadi.

Uhaba wa vyakula nchini humu umehusishwa na masuala mbalimbali, baadhi ya wataalamu wakidai viongozi walio serikalini huwa hawana nia ya kutatua matatizo aina hii kwa sababu zao za kibinafsi.

Uagizaji wa vyakula kutoka nchi za nje ni mojawapo ya biashara kubwa ambazo zinafahamika kuvutia wafanyabiashara wenye ushawishi wakiwemo wanasiasa.

Bidhaa ambazo zimevutia mabwanyenye wengi ni kama vile unga wa ngano, ule wa mahindi, sukari na mchele.

Hii ni licha ya kuwa hizi ni bidhaa ambazo zinaweza kufanya vyema humu nchini maadamu kuna rotuba za kutosha za kilimo cha mazao hayo.

Hivyo basi, mtu yeyote hatakuwa amekosea kubahatisha kuwa kuna kusudi la wengi walio mamlakani kukataa kutafuta suluhisho la kudumu kwa uhaba wa chakula unaokumba nchi hii kila mara.

Tunahitaji pawepo viongozi ambao watajitolea kikamilifu kutatua matatizo ya kimsingi yanayokumba raia, na pia mengine mengi yanayoibuka kadri na jinsi miaka inavyosonga.

Tutakuwa katika hali mbaya iwapo katika miaka inayokuja, tutakuwa bado tunazungumzia changamoto hizi za jadi wakati ambapo mataifa mengine yaliyokuwa nyuma yetu yakishughulikia masuala muhimu ya kisasa.

Kenya ina uwezo wa kutosha kutekeleza mipango ambayo itaboresha maisha ya umma katika nyanja tofauti na kile kinachohitajika ni viongozi wasio na ubinafsi.

Hii itahitaji wananchi kufanya maamuzi ya busara ili wapate viongozi wanaojali maslahi yao.

You can share this post!

Ruto na Matiang’i wavutania machifu

Wavenezuela: Chebukati abaki kimya

T L