• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 8:55 PM
Ruto na Matiang’i wavutania machifu

Ruto na Matiang’i wavutania machifu

NA VALENTINE OBARA

NAFASI ya machifu katika maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9 inazidi kuibua hisia mseto baina ya viongozi serikalini na wanasiasa huku serikali ikitangaza kuongeza maeneo ya kiutawala katika kaunti 16.

Wanasiasa wa mrengo wa Kenya Kwanza wakiongozwa na Naibu Rais William Ruto, wamekuwa wakidai kwamba kuna njama ya serikali kutumia maafisa hao wa utawala kwa maslahi ya Kiongozi wa ODM, Raila Odinga, anayewania urais kupitia chama cha Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya.

Hata hivyo, madai haya yamepingwa na serikali kupitia kwa Wizara ya Usalama inayosimamiwa na Fred Matiang’i, ambaye ni mmoja wa mawaziri wanaohusishwa na kampeni za Azimio.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara wikendi, mgombea mwenza wa Dkt Ruto katika uchaguzi wa urais, Rigathi Gachagua, aliendeleza madai kwamba maafisa wa utawala wanashinikizwa kutumia mamlaka yao kushawishi jinsi raia watakavyopiga kura Agosti 9.

Naye Dkt Matiang’i akiwa katika Kaunti ya Nyamira wikendi, alisisitiza wataendelea kufanya mikutano na machifu na maafisa wengine wa utawala kwa maandalizi ya uchaguzi kwa vile wana majukumu muhimu.

“Tukikutana na hawa machifu ni kwa sababu tunataka kupanga kazi. Ni kazi tunapanga ili kuhakikisha nchi yetu ina amani, watu wetu wanakaa kwa umoja na tunamaliza huu uchaguzi bila matatizo yoyote,” akasema Dkt Matiang’i.

Katibu wa Wizara ya Usalama, Dkt Karanja Kibicho, aliyekuwa ameandamana naye, alisisitiza watumishi wa umma wana haki ya kushauri umma kuhusu viongozi wanaostahili kuwachagua.

Mvutano huu unajiri Dkt Matiang’i akichapisha kwenye gazeti rasmi la serikali amri ya kuunda kaunti ndogo, lokesheni na lokesheni ndogo, katika baadhi ya kaunti zilizo maeneo ya Nyanza, Magharibi, Pwani, Mashariki na Kaskazini Mashariki.

Hatua hii ya wiki iliyopita inatarajiwa kupelekea ongezeko la maafisa wa utawala wakiwemo machifu na manaibu wao.

Dkt Matiang’i alisema, hatua ya kubuni maeneo mapya ya kiutawala inalenga “kuboresha uratibu wa majukumu ya serikali ya kitaifa”.

Katika Kaunti ya Migori, kulibuniwa Kaunti Ndogo ya Nyatike Magharibi ambayo itakuwa na divisheni za Kanyasa na Kachieng.

Kaunti Ndogo ya Nyatike itakuwa na kata za Karungu Kusini, Karungu Kaskazini na Ungoe, huku kukiwa na kata ndogo za Rabare, Omange, Wachara na Wang’aya.

Kata ndogo ya Okayo imegawanywa ili kuwe na Lower Okayo na Upper Okayo.

MAENEO MAPYA

Kaunti ya Homa Bay itakuwa na kata ndogo za Kanyalganda, Wayara na Sibuoche katika kata ya Kadhola, Kaunti Ndogo ya Ndhiwa.

Kaunti Ndogo ya Rangwe nayo itakuwa na kata ndogo za Katolo na Lower Kanyaruanda na kata ya Kagan Kaskazini.

Kaunti nyingine za Nyanza na Magharibi zilizopewa maeneo mapya ya kiutawala wa serikali ni Kisumu, Busia, Vihiga na Kakamega.

Katika Kaunti ya Kericho, serikali imesema kuwe na kata ndogo za Menet, Chagoror na Saoset na Ng’omwo katika Kaunti Ndogo ya Kipkelion, ambapo pia kata ya Sugutek imebadilishwa jina iwe Kalyet.

Kutakuwa na kata mbili ambazo ni Timbilil na Kutung.Kaunti ya Nandi itakuwa na kata ndogo za Kipletito na Kaptien, kata ya Keburo, Kaunti Ndogo ya Nandi Mashariki huku Narok ikiwa na kata ndogo za Sekerot na Emeterai katika kata ya Enooseyia iliyo Kaunti Ndogo ya Narok Mashariki.

Kaunti ya Baringo itakuwa na kata ndogo ya Tabarin katika Kaunti Ndogo ya Baringo ya Kati.

Katika Kaunti ya Tharaka Nithi, kutakuwa na Kaunti Ndogo za Chuka Kaskazini na Chuka Kusini, huku Lamu kukiwa na kata ndogo za Mbwajumwali na Kengevani katika kata ya Vumbe, Kaunti Ndogo ya Lamu Mashariki.

Kaunti ya Machakos itakuwa na kata ndogo ya Myland katika Kaunti Ndogo ya Athi River.Katika ukanda wa Kaskazini Mashariki, Kaunti ya Garissa imepata kata ndogo za Kunaso na Baashal katika Kaunti Ndogo ya Garissa.

Dkt Matiang’i ameagiza kuwe na kata ndogo ya Liban, kata ya Wel Ari katika Kaunti Ndogo ya Habaswein iliyo Wajir.

Kaunti hiyo itakuwa pia na kata ndogo za Abaq Haluul na Findigo katika kata ya Abaqmadobe, Kaunti Ndogo ya Diff.

Kaunti jirani ya Mandera itakuwa na kata ndogo za Jibal na Murat-elow katika Kaunti Ndogo ya Banisa.

  • Tags

You can share this post!

Kijiji cha Tana River ambapo kutongozana ni haramu kubwa

TAHARIRI: Uhaba huu wa vyakula ni fedheha kwa Kenya

T L