• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
TAHARIRI: Ushirikiano wa Kenya, Tanzania usiwe mdomo tu

TAHARIRI: Ushirikiano wa Kenya, Tanzania usiwe mdomo tu

NA MHARIRI

HATUA ya marais wa Kenya na Tanzania kuamua kukamilisha makubaliano ya awali kati ya nchi hizi mbili, itasaidia kuharakisha kuondoa vikwazo ambavyo vimekuwepo kwa miaka mingi.

Nchi za Kenya na Tanzania zina uwezo wa kufaidi kiuchumi na hivyo basi kuinua hali ya maisha ya wananchi ikiwa vikwazo vingi vilivyopo vitaondolewa kabisa.

Wananchi wa mataifa haya mawili hasa wanaoishi mipakani, sawa na nchi nyingine jirani kama vile Uganda huwa wanaishi kama ndugu na dada na hawatambui mipaka iliyopo kati yao.

Hata hivyo, ifikapo katika masuala ya usimamizi na biashara zinazohitaji mchango wa asasi za serikali ndipo tofauti nyingi huibuka kwa sababu ya urasimu na ushindani uliopo kimataifa.

Katika miaka iliyopita, juhudi nyingi zilikuwa zikiwekwa kujaribu kuondoa vikwazo ambavyo vinatatiza uwezo wa nchi hizi mbili kushirikiana kwa njia inayoweza kuwa kwa manufaa ya wananchi, wafanyabiashara na wadau wa sekta nyingine zote muhimu.

Hata hivyo, inavyoonekana, kila utawala mpya unapoingia huwa kuna mikakati mipya inayowekwa kutafutia suluhu changamoto zile zile za tangu jadi.

Wakati huu, kuna matumaini kwamba Rais William Ruto wa Kenya na mwenzake wa Tanzania, Rais Samia Suluhu, wamejitolea kukamilisha utekelezaji wa makubaliano ambayo yalikuwa yamewekwa awali.

Katika ziara yake nchini humo jana Jumatatu, Rais Ruto alibainisha kuwa walijadiliana kuhusu masuala mengi yaliyo na umuhimu kwa maendeleo ya mataifa hayo mawili.

Miongoni mwao ni kuhusu biashara, usalama mipakani, utalii miongoni mwa mengine.

Kilichojitokeza wazi ni jinsi walivyosisitiza hitaji la kukamilisha makubaliano ambayo Rais Samia alikuwa ameweka awali na aliyekuwa rais Uhuru Kenyatta.

Wawili hao walipokutana Nairobi mwaka uliopita, waliamua kuunda jopo la mawaziri na maafisa wakuu serikalini wa nchi hizo mbili.

Jopo hilo lilikuwa na jukumu la kuchunguza na kupendekeza suluhisho za kuondoa vikwazo ambavyo vimekuwa vikiathiri vibaya biashara na ushirikiano wa Kenya na Tanzania.

Ikizingatiwa kuwa rasilimali nyingi na muda ushatumiwa katika jopo hili, nchi hizi mbili zijitolee kumaliza kazi iliyoanzishwa hata kama serikali ya Kenya sasa ni mpya na inatarajiwa kuwa na mawaziri wapya hivi karibuni.

Hatua hii haitasaidia tu kuokoa rasilimali za umma, bali itaokoa pia muda wa kuondolea wananchi na wawekezaji vikwazo vinavyowazuia kusonga mbele katika shughuli zao zinazogusia nchi hizo.

You can share this post!

Urusi yaua raia wengi wa Ukraine kwa kisasi

CHARLES WASONGA: Wabunge wa Kenya Kwanza wafaa kujua wao si...

T L