• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 3:21 PM
Urusi yaua raia wengi wa Ukraine kwa kisasi

Urusi yaua raia wengi wa Ukraine kwa kisasi

NA MASHIRIKA

ANKARA, UTURUKI

ZAIDI ya watu wanane walifariki Jumatatu katika jiji kuu la Ukraine, Kyiv, baada ya Urusi kurusha makombora katika miji kadhaa nchini humo, zilisema idara za serikali.

Kulingana na Wizara ya Usalama wa Ndani nchini humo, jumla ya watu 24 walijeruhiwa katika eneo la Shevchenkivski, lililo viungani mwa Kyiv.

Awali, Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky alithibitisha uwepo wa maafa kutokana na mashambulio hayo, huku akiwarai wakazi kukaa majumbani mwao.

Msururu wa milipuko uliripotiwa katika miji ya Zhytomyr, Khmelnytsky, Dnipro, Lviv, Ternopil na Kyiv.

Mashambulio hayo yanatokea siku moja baada ya Rais Vladimir Putin wa Urusi kuikashifu Ukraine kwa “shambulio la kigaidi” dhidi ya Daraja la Kerch.

Daraja hilo ndilo la pekee linaloiunganisha Urusi na eneo la Crimea, ililoliteka kutoka kwa Ukraine mnamo 2014.

“Mbinu pekee ya Putin ni kutekeleza mashambulizi katika miji yenye amani nchini mwetu. Hata hivyo, hatutatishika hata kidogo,” akasema Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Ukraine, Dmytro Kuleba, kupitia mtandao wa Twitter.

Vyombo vya habari nchini humo viliripoti kuwa huduma zote za uchukuzi wa reli zilisimamishwa jijini Kyiv kutokana na mashambulio hayo.

Kulingana na meya wa Kyiv, Vitali Klitschko, jiji hilo bado linakabiliwa na tishio kubwa la kiusalama kutokana na mashambulio hayo.

Alisema kuwa barabara kuu jijini humo zimefungwa na vikosi vya usalama huku shughuli za uokozi zikiendelea.

Baadaye, Wizara ya Usalama wa Ndani ilisema kuwa kombora moja lililorushwa na Urusi lilianguka katika barabara ambako afisi za Rais Zelensky zipo.

Msaidizi mkuu wa Rais Zelensky, Mykhailo Podolyak, alisema kuwa mashambulio dhidi ya miji hiyo inaonyesha “nia ya Urusi kuendeleza ugaidi wake”.

Rais Putin alitarajiwa kufanya mkutano wa baraza lake la usalama hapo jana.

Wakati huo huo, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Ukraine, Dmytro Kuleba, amelazimika kukatiza ziara yake katika mataifa kadhaa barani Afrika kutokana na mashambulio yanayoendelezwa na Urusi.

“Ninawasiliana na maafisa wakuu serikalini kufahamu hali ilivyo nchini mwetu.Itanilazimu kurudi ili kushirikiana nao kubuni mikakati ya kujibu na kudhibiti mashambulio ya Urusi. Ninarejea mara moja,” akasema jana, kwenye ujumbe alioweka kwenye mtandao wa Twitter.

Waziri huyo amekuwa katika juhudi za kuirai Afrika kuiunga mkono Ukraine.

Ziara yake inafuatia ziara kama hiyo iliyofanywa na Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Urusi, Sergei Lavrov mnamo Julai.

Kabla ya kukatiza ziara hiyo, waziri huyo alikuwa amezuru nchi za Senegal, Ivory Coast na Ghana.

Rais Zelensky amekuwa akiwarai viongozi kutoka Afrika kuiunga mkono nchi yake kuikashifu Urusi kutokana na uvamizi dhidi ya Ukraine.

  • Tags

You can share this post!

Barcelona wakung’uta Celta Vigo na kurejea kileleni...

TAHARIRI: Ushirikiano wa Kenya, Tanzania usiwe mdomo tu

T L