• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
TAHARIRI: Ushuru zaidi ni sawa ila sharti mianya yote ya wizi izibwe

TAHARIRI: Ushuru zaidi ni sawa ila sharti mianya yote ya wizi izibwe

NA MHARIRI

RAIS William Ruto wiki jana ameelekeza Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru nchini (KRA), kuhakikisha kuwa inafikisha pato la angaa Sh3 trilioni katika kipindi cha kifedha cha mwaka huu.

Naam, shabaha hiyo iko juu zaidi na huenda isiwezekane ikizingatiwa kuwa mwaka uliopita wa kifedha KRA ilifanikiwa kukusanya Sh2 trilioni pekee.

Hakika ongezeko la Sh1 trilioni katika mwaka mmoja pekee ni jambo gumu zaidi kutekelezwa.Ongezeko la asilimia 50 katika miezi 12 pekee ni sawa na ndoto.

Hata hivyo, ni muhimu kulenga juu zaidi ndipo juhudi zifanywe kuhakikisha kuwa ushuru unapatikana kwa wingi. Yamkini KRA itafaulu kukusanya Sh500 bilioni zaidi ambazo ni sawa na nusu trilioni au asilimia 25 zaidi ikilinganishwa na mwaka wa kifedha uliopita.

Inapozingatiwa kuwa bajeti ya Kenya katika mwaka ni Sh3.2 trilioni, iwapo KRA itafanikiwa kukusanya Sh2.5 trilioni, basi serikali haitalazimika kukopa sana kutoka kwa wakopeshaji ili kujaza pengo litakalokuwa kwenye bajeti yake. Itahitajika kukopa Sh700 bilioni pekee kinyume na sasa ambapo taifa hukopa takribani Sh1 trilioni kila mwaka.

Msukumo katika hali hii ni kuhakikisha kuwa serikali inapunguza deni lake kwa kiwango kikubwa huku ikifanikisha maendeleo. Inapozingatiwa kuwa tayari deni la jumla la taifa hili linaelekea Sh9 trilioni, pana haja ya kupunguza sana ukopaji au hata kuepuka kukopa kabisa, hata iwapo hatua hiyo itamaanisha baadhi ya miradi ya maendeleo kukwama.

Ili kufanikisha pato kubwa la nchi kupitia KRA, serikali inahitajika kuhakikisha kuwa wakwepaji wote wa ushuru wanaandamwa na kulazimishwa kulipa uhuru, au hata kuongeza viwango vya ushuru vinavyotozwa Wakenya kwa sasa.

Lakini inapozingatiwa kuwa gharama ya maisha ni kubwa sana kiasi cha kuanza kuwalemea baadhi ya raia, njia aula ya kufanikisha lengo kama hili ni ‘kumlazimisha’ kila mtu anayestahili kulipa ushuru kufanya hivyo badala ya kumuongeza raia wa kawaida kodi.

Mbali na hilo, imekadiriwa kuwa katika pato hilo la mwaka, angaa thuluthi yake, sawa na Sh600 bilioni huibwa na watu waliotwikwa jukumu la kuwahudumia Wakenya.

Hivyo basi, ni muhimu sana kwa serikali ya Rais Ruto kuwahakikishia raia kwa dhati kuwa hakuna pesa yoyote ya mlipa-ushuru itakayopotea. Vinginevyo, juhudi zake hizo zote zitakuwa kazi bure. Tulipe ushuru tuweze kujitegemea badala ya kutegemea wakopeshaji.

You can share this post!

Mikakati ya UDA kumaliza Kalonzo

Leo siku ya mwisho kupeleka maombi kwa Bunge la EALA

T L