• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 6:07 PM
Mikakati ya UDA kumaliza Kalonzo

Mikakati ya UDA kumaliza Kalonzo

NA PIUS MAUNDU

CHAMA cha United Democratic Alliance (UDA) kimeweka mikakati ya kumzima kinara wa Wiper, Kalonzo Musyoka anayeonekana kuwa tishio kwa Rais William Ruto katika uchaguzi wa 2027.

Miongoni mwa mikakati hiyo ni kuanzisha kampeni kali dhidi ya Bw Musyoka katika eneo la Ukambani na kuzima wandani wake kuhudhuria hafla za kugawa chakula cha msaada kwa waathiriwa wa njaa katika kaunti tatu za eneo hilo.

Mipango ya kumaliza ushawishi wa Bw Musyoka Ukambani na maeneo mengine ya nchi, iliafikiwa katika mkutano uliofanyika Jumapili nyumbani kwa mwenyekiti wa UDA Johnson Muthama Kaunti ya Machakos.

Mkutano huo ulihudhuriwa na wandani wa Rais Ruto wanaojumuisha wasomi na wanasiasa waliopoteza viti katika Uchaguzi wa Agosti 9.

Chama cha UDA kinahofia kuwa huenda Bw Musyoka akaungwa mkono na kinara wa Azimio, Raila Odinga na Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta na kuhangaisha Rais Ruto katika uchaguzi mkuu ujao.

“Maafisa wa serikali wamehimizwa kuandamana na wanasiasa wa Kenya Kwanza wanapogawa chakula cha msaada kwa waathiriwa wa njaa na hata kuzindua miradi ya maendeleo inayofadhiliwa na serikali,” akasema Bw Muthama.

Kaunti za eneo la Ukambani – Kitui, Machakos na Makueni – ni miongoni mwa kaunti zilizoathiriwa zaidi na baa la njaa.Viongozi wa UDA wanahisi kuwa kumruhusu Bw Kalonzo kuhudhuria hafla ya kugawa chakula kutamuongezea umaarufu.

Kalonzo ambaye alikuwa ameahidi kuanza kampeni zake za urais mara baada ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Agosti 9, amekosoa serikali kwa kutumia chakula cha msaada kujipigia debe.

Jumamosi, wandani wa Bw Kalonzo – Gavana wa Makueni, Bw Mutula Kilonzo Junior na mbunge wa Makueni, Bi Suzanne Kiamba – walihudhuria hafla ya kugawa chakula iliyoongozwa na mke wa Naibu wa Rais Rigathi Gachagua, Dorcas.

“Hatuwezi kuruhusu viongozi wa Azimio kukosoa serikali ilhali wanahudhuria hafla za ugavi wa chakula cha msaada na uzinduzi wa miradi ya maendeleo ya serikali,” Bw Muthama aliambia Taifa Leo.

Viongozi wa UDA kutoka Ukambani pia watapanga kuanzisha kampeni kali dhidi ya Kalonzo kwa lengo la kumaliza umaarufu wake.

Wataeleza wakazi wa eneo hilo kuwa Bw Musyoka hana nafasi ya kushinda urais, kulingana na aliyekuwa Seneta wa Kitui, Bw David Musila.

“Jamii ya Wakamba itaendelea kuwa upinzani iwapo itaendelea kuunga mkono Kalonzo. Jamii haina budi kuunga mkono serikali ya Kenya Kwanza ili tunufaike kwa maendeleo,” akasema Bw Musila.

Wanasiasa hao wa Kenya Kwanza wameapa kuhakikisha kuwa jamii ya Wakamba – katika eneo la Ukambani, Nairobi na Mombasa – wanaunga mkono Rais Ruto.

Viongozi hao wanadai kuwa Bw Musyoka ndiye aliyekataa kutengwa kwa Mwingi kuwa kaunti iliyojitegemea kutoka kwa Kaunti ya Kitui.

Kulingana nao, hatua hiyo ilisababisha wakazi wa Mwingi – ambapo ni nyumbani kwa Kalonzo – kukosa huduma muhimu.

Wanasiasa hao pia wametwikwa jukumu la kupigia debe serikali ya Kenya Kwanza huku wakishawishi wakazi kuunga mkono Rais Ruto.

“Idadi ya wakazi wa Ukambani wanaounga mkono Rais Ruto imeanza kuongezeka, ishara kwamba anakubalika,” akasema Bw Muthama.

Rais Ruto tayari amemfungulia mlango Bw Musyoka huku akisema kuwa yuko tayari kufanya kazi naye iwapo atabadili nia.

Rais Ruto mwezi uliopita pia alifichua kuwa alijaribu kumshawishi Kalonzo kufanya naye kazi bila mafanikio.

Bw Muthama, hata hivyo, jana Jumatatu alisema kuna uwezekano mkubwa Bw Musyoka atafanya kazi na Rais Ruto katika siku za usoni.

Kalonzo amekuwa akizunguka katika maeneo yanayoaminika kuwa ngome za muungano wa Azimio katika hali inayofasiriwa na wadadisi kuwa huenda ameanza kampeni za 2027.

Kiongozi wa Wiper wiki iliyopita alitangaza kuwa muungano wa Azimio utatangaza ‘baraza la mawaziri’ wa upinzani watakaokabili serikali ya Kenya Kwanza.

Wadadisi wa masuala ya kisiasa wanaonya kuwa Bw Musyoka ataisha kisiasa iwapo atakubali kupewa wadhifa serikalini na Rais Ruto. Wandani wa Rais Ruto, hata hivyo, wanataja kuwa huenda mpango wao wa kuzima Bw Musyoka Ukambani ukaambulia patupu iwapo hawataungana.

Wanasiasa wa eneo la Ukambani wanaounga mkono Rais Ruto wamegawanyika katika makundi mawili – kundi moja linaongozwa na Bw Muthama huku jingine likiongozwa na waziri wa Mashauri ya Kigeni Alfred Mutua.

Aliyekuwa Gavana wa Makueni Kivutha Kibwana na aliyekuwa mbunge wa Mwingi ya Kati Joe Mutambu wameonya kuwa kambi hizo mbili zisipoungana huenda wakashindwa kumaliza umaarufu wa Bw Musyoka katika eneo la Ukambani.

  • Tags

You can share this post!

Rais wa zamani Da Silva ashinda tena urais Brazil

TAHARIRI: Ushuru zaidi ni sawa ila sharti mianya yote ya...

T L