• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
TAHARIRI: Vikosi vya Kenya michezo ya shule Tanzania vijikaze kudumisha ubabe

TAHARIRI: Vikosi vya Kenya michezo ya shule Tanzania vijikaze kudumisha ubabe

NA MHARIRI

MICHEZO ya Shule za Upili ya Muhula wa Pili katika ngazi ya kanda inaingia siku ya pili, leo katika uga wa Tanzania Game and Track, mjini Arusha, Tanzania na jana kulikuwa na matokeo mseto.

Kwenye mechi za ufunguzi katika makundi mbalimbali, Moi Girls Kamusinga walifaulu kujipatia ushindi kwenye mpira wa mkono 34-22 dhidi ya wenyeji Katoro huku magwiji katika mchezo wa voliboli kwa wasichana Kwanthanze wakipata pia ushindi muhimu wa seti 3-0 dhidi ya Katikamu SDA ya Uganda.

Hata hivyo, katika vitengo vya soka na basketiboli, timu za Kenya zilipata sare na kuchapwa, mtawalia.

Ama kwa kweli wadau wengi wanakubaliana kwamba kwa makala hii, timu za Kenya zimewekwa kwenye makundi magumu katika vitengo vyote wanavyowakilisha ikiwemo michezo ya soka, basketiboli, voliboli, handiboli, netiboli, raga na hoki.

Mara ya mwisho kipute hiki kilipofanyika mwaka wa 2019, ambapo ilikuwa kabla ya janga la corona kubisha hodi katika pande hii ya dunia, Kenya ilijipatia ubingwa katika voliboli ya wasichana kupitia timu ya Kwanthanze Secondary.

Moi Girls Kamusinga nao walifaulu kubeba taji la handiboli huku Kakamega High wakichukua taji la raga ya wachezaji 15 nao Upper Hill wakaondoka na taji la raga ya wachezaji 7 kila upande.

Hata hivyo, kwa jumla, Uganda walifaulu kuipiku Kenya kwenye thamani ya medali licha ya kutoshana kwa medali 27 kila moja ingawa Uganda ikawa na dhahabu moja zaidi (11) kuliko Kenya (10) matokeo ya mwisho yalipotangazwa.

Ni kwenye pazia hili, la kulikosa taji pembamba ambapo washiriki wanachangamkia michezo hiyo Arusha kwa mwaka huu na ni matarajio ya mashabiki na Wakenya kwa jumla kwamba vikosi vyetu vimefanya mazoezi na utathmini wa kutosha kufaulu kutoa ushindani mkali na kurejea nyumbani na taji mara hii.

Kama safu hii inavyosisitiza kila wakati, michezo ni sehemu kubwa ya maisha ya kisasa ya maendeleo ya talanta na utandawazi na ni majukwaa makubwa kama haya ya kanda ya Afrika Mashariki ambayo inajumuisha Kenya, Uganda, Tanzania na Rwanda ndipo vipaji vipya hutambulika na kukwezwa.

Kwa sababu hiyo, inapaswa kwamba shule zote washiriki zipange mikakati ya kuhakikisha kwamba wanaonyesha ufundi wa hali ya juu. Kwa kipute hicho kinachoendelea kwa sasa, wito wetu ni wa kuwatia shime na kupambana vilivyo na upinzani na kuletea taifa medali kochokocho. Kila la heri kwa wote!

You can share this post!

Madai ya kuteua wapenzi, jamaa yakumba uteuzi wa madiwani...

Faida za ulaji wa tunda la tini

T L