• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 8:55 PM
TAHARIRI: Wanasiasa wadumishe nidhamu katika siasa

TAHARIRI: Wanasiasa wadumishe nidhamu katika siasa

NA MHARIRI

KENYA imechukua mkondo mbaya wa kupiga siasa chafu katika kampeni zake.

Uhasama unaodhihirika sasa hivi katika kampeni za mirengo mbalimbali hasa katika kinyang’anyiro cha urais zinaisawiri nchi hii kama isiyojua ustaarabu wowote.

Mwenendo wa wawaniaji wengi umekuwa ule wa matusi, uchochezi na siasa chafu kwa jumla. Je, ni lini tutajifunza kutokana na mataifa yaliyokomaa kidemokrasia kama vile Amerika na Uingereza?

Ni jambo la kawaida kuwasikia washindani wakitupiana maneno yasiyokuwa ya adabu kama vile kuitana ‘yule mganga’ , ‘yule mtu wa vitendawili’ au ‘yule mwizi ama ‘yule Arap Mashamba’.

Kwa hakika huku ni kukosa adabu kabisa na mfano mbaya usiofaa kuigwa. Hiyo ni siasa chafu inayodunisha hadhi ya mtu anayetarajiwa kuwa rais wa taifa hili.

Ukifuatilia kampeni za Amerika, kwa mfano, utasikia wawaniaji wanaoshindana wakishindana kwa sera badala ya kutukanana jinsi inavyoshuhudiwa hapa kwetu.

Kwa mfano, utamsikia mwaniaji mmoja wa Amerika akiwaambia wafuasi wake kuwa, “Iwapo mnataka udikteta basi chagueni wapinzani wetu.”

Ukitazama kauli hiyo kwa makini, utabaini kuwa wanasiasa hao wameshambuliana japo kwa kulenga hoja – katika muktadha huu, mpinzani wanayemrejelea ana sifa za udikteta bali si kumuita mpinzani huyo dikteta moja kwa moja.

Wazo hili linafaa liwachochee wanasiasa wetu kutumia mbinu nzuri katika kampeni. Wakenya wanahitaji kuwaona wawaniaji wakijiepusha na matusi, uhasama na chuki na badala yake washindane kwa hoja na sera.

Kwa hivyo, kama njia ya kuwatia adabu wanasiasa hao waliozoea kurushiana cheche zisizofaa, wapigakura wanatiwa shime wawanyime kura ili liwe funzo kwao.

Wapigakura watekeleze wajibu wao ifaavyo kwa kuwapigia wanasiasa wenye nidhamu pekee katika uchaguzi mkuu ujao.

Kasumba ya kugawanya Wakenya kwa misingi ya kikabila au tabaka kwa madhumuni ya kujizolea kura sharti itokomezwe mara hii ndipo tutajivunia taifa lililokomaa kidemokrasia.

Kwa mantiki hiyo, aidha, ni makosa baadhi ya wanasiasa kupanga vitendo vya kihuni ili kuvuruga mikutano ya wenzao kama inavyoshuhudiwa katika baadhi ya maeneo wanakozuri wanasiasa hao wanaosaka viti hapo Agosti.

You can share this post!

Majibizano makali yaendelea kuhusu matamshi ya Ruto

Fedha: Wakuu wa shule sasa waingia baridi

T L