• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 9:01 PM
Majibizano makali yaendelea kuhusu matamshi ya Ruto

Majibizano makali yaendelea kuhusu matamshi ya Ruto

BRIAN OJAMAA Na WYCLIFFE NYABERI

VIONGOZI wa chama cha DAP-K wamemkashifu vikali Naibu Rais William Ruto kuhusiana na matamshi aliyotoa Jumanne dhidi ya Waziri wa Ulinzi Eugene Wamalwa akimlinganisha na mwanamke.

Walisema Alhamisi mjini Bungoma kwamba matamshi hayo hayafai, na huenda yakasababisha machafuko kabla na baada ya uchaguzi mkuu wa Agosti.

Alipokuwa akifanya kampeni Jumanne katika Kaunti za Bungoma na Trans Nzoia, Dkt Ruto alikanusha madai kuwa alitaka kumzaba kofi Waziri Wamalwa.

Alisema kwamba jamii ya Kalenjin hairuhusu wanaume kuwazaba makofi wanawake, akimrejelea Bw Wamalwa.

Matamshi hayo yalipokewa kwa hisia kali kutoka kwa wadau mbalimbali, wakiwemo watu wa jamii ya Waluhya.

Walimshutumu Dkt Ruto kwa kuidhalilisha ‘jamii nzima’.

Wakihutubia wanahabari Alhamisi katika kilabu kimoja mjini Bungoma, viongozi hao wakiongozwa na kinara wa DAP-Kenya, Bw Wafula Wamunyinyi, walisema matamshi hayo yanawavunjia heshima wanawake na watu wa jamii anayotoka waziri Wamalwa kwa ujumla.

“Tunataka kukashifu matamshi ya chuki yaliyotolewa na Dkt Ruto dhidi ya viongozi wa nchi hii. Tumekuwa tukifuatilia kwa makini matamshi yake ya awali. Tumegundua amekuwa akiwarushia matusi Rais Uhuru Kenyatta, Raila Odinga na sasa amemgeukia mtoto wetu Wamalwa. Hilo si jambo zuri kwa kiongozi wa hadhi yake,” akasema.

Mbunge huyo wa Kanduyi alidai Dkt Ruto ana matatizo ya kudhibiti hasira, yanayohitaji kuchunguzwa.

Bw Wamunyinyi alisema mnamo Jumatano, Dkt Ruto alimgombeza vikali kijana mmoja katika mkutano Kaunti ya Vihiga kwa sababu ni mfuasi sugu wa Azimio One Kenya.

Mbunge huyo alisema Dkt Ruto anapaswa kujua Waluhya hawajafurahishwa na matamshi yake ya kumfananisha Wamalwa na mwanamke.

“Nataka kuwahimiza Wakenya kuangazia jinsi Ruto anawatukana viongozi. Msimpe nafasi ya kuongoza taifa hili. Kama kiongozi wa DAP-Kenya, nataka kukashifu matusi ya Ruto kwa viongozi wenzangu, na jinsi anavyojipiga kifua hadharani bila nidhamu kama naibu rais wa nchi hii,” alisema.

Shutuma sawa na hizo zilitolewa na Bw Odinga Jumatano akiwa katika mkutano wa kisiasa Kaunti ya Kwale.

“Ati Dkt Ruto anatusi waziri anayefanya kazi naye. Anasema ati yeye ni mwanamke. Yeye alijuaje yeye ni mwanamke? Hii hasira yake sisi hatuitaki. Hasira ni hasara,” alisema Bw Odinga.

Mgombea mwenza wa Bw Odinga Bi Martha Karua alisema matamshi ya Dkt Ruto ni ya kudhalilisha akina mama.

“Bw Odinga anawaheshimu akina mama na sio kama wapinzani wetu. Unapomkosea heshima waziri ambaye mko katika serikali moja, je mwananchi wa kawaida? Angalieni kiongozi kwa tabia yake,” akasema Bi Karua.

Kulingana na gavana wa Kitui Charity Ngilu, matamshi ya Dkt Ruto ni ya kuwadhalilisha wanawake. Katibu Mkuu wa Muungano wa vyama vya wafanyakazi nchini (COTU), Bw Francis Atwoli alidai hatua ya Dkt Ruto kumtukana Bw Wamalwa nyumbani kwao ni matusi kwa jamii nzima.

  • Tags

You can share this post!

TUSIJE TUKASAHAU: Kilio cha familia za wahanga wa ajali ya...

TAHARIRI: Wanasiasa wadumishe nidhamu katika siasa

T L