• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 1:57 PM
VALENTINE OBARA: Piga kura uchaguzini, usipige domo kuhusu dhuluma chamani

VALENTINE OBARA: Piga kura uchaguzini, usipige domo kuhusu dhuluma chamani

NA VALENTINE OBARA

LALAMA zinazidi kuenea kuhusu mbinu ambazo vyama vikuu vilitegemea sana kuchagua wagombeaji viti wa uchaguzi ujao katika pembe mbalimbali za nchi.

Tofauti na jinsi ilivyokuwa katika miaka iliyopita ambapo vyama vikuu vilitumia kura za mchujo kuamua wagombeaji, hali imekuwa tofauti mwaka huu.

Eneo la Pwani ni mojawapo ya sehemu za nchi ambapo idadi kubwa ya viongozi watakaowania viti katika uchaguzi ujao kupitia kwa vyama vya kisiasa wamepewa tikiti za moja kwa moja.

Malalamishi mengi yametolewa kuhusu mfumo huo wa kuteua wagombeaji lakini lalama inayojitokeza zaidi hadi sasa ni kuhusu suala la ulinzi wa demokrasia.

Baadhi ya walalamishi wanadai kuwa, kwa kuteua wagombeaji moja kwa moja bila kupitia kwa kura ya mchujo, wananchi wamenyimwa nafasi ya kujiamulia viongozi wanaowataka.

Kwa kiwango fulani, tetesi hii ina mashiko ila kwa mtazamo wa kina zaidi, utagundua kuwa wananchi wana sababu finyu ya kulalamikia ukandamizaji wa demokrasia katika vyama vya kisiasa.

Wakenya wamebahatika kuwa na Katiba ambayo imewapa wanasiasa nafasi ya kuwania viti kama wagombeaji huru wasiotegemea vyama vya kisiasa.

Hii ni kumaanisha kuwa, wale wote wanaolalamika kunyimwa nafasi ya kutimiza haki zao za kidemokrasia wana nafasi ya kutimiza haki hiyo debeni wakati wa Uchaguzi Mkuu.

Ikiwa kweli unaamini wewe ni kiongozi bora anayestahili kupewa nafasi mamlakani, basi huna budi ila kuwa mgombea huru endapo vyama vya kisiasa vimekudhulumu.

Kwa msingi uo huo, kama wewe ni mfuasi wa chama ambacho unaamini hakikutenda haki katika mchujo, uhuru ni wako kujiamulia kiongozi bora unayemtaka bila kushurutishwa na chama chako.

Vigogo wa kisiasa walianza mapema kuwahimiza raia kupigia kura viongozi wote wa chama kimoja katika uchaguzi ujao, mtindo ulio maarufu kama ‘kura ya suti’.

Hata hivyo, raia mwenye busara ambaye kweli anaamini kunahitajika viongozi bora katika eneo lake, atafanya uamuzi wake uchaguzini kwa kuzingatia uwezo wa wagombeaji binafsi bila kujali vyama vyao.

Katika Uchaguzi Mkuu uliopita, kuna wanasiasa ambao waliaminika wangelishinda viti kwa sababu waliwania kupitia kwa vyama fulani maarufu maeneo yao, wakaungwa mkono na vigogo wa kisiasa huku wakiwa na rasilimali tele za kampeni lakini wakabwagwa na wagombeaji huru.

Matukio hayo yalidhihirisha kuwa, nafasi ya raia kutimiza jukumu lake la kidemokrasia uchaguzini haiishi katika kura ya mchujo wa vyama.

Uchaguzi ujao unatarajiwa kuwa na idadi kubwa ya wagombeaji huru.

Huu utakuwa mtihani kwa wananchi wanaolalamikia hitaji la uongozi bora kuthibitisha nia yao kwa kutumia nguvu zao za kikatiba kujiamulia ipasavyo.

Inaeleweka kuwa, wagombeaji wanaotumia vyama vya kisiasa hasa vyama vikuu vilivyo na umaarufu mkubwa huwa wana nafasi bora ya ushindi.

Hii ni kutokana na uwezo wa wagombeaji hao kupata usaidizi wa kujivumisha kutoka kwa wanasiasa mashuhuri walio nao chamani.

Kando na hayo, vyama vya kisiasa huwa na rasilimali tele za kupenya mashinani kutafuta uungwaji mkono ikilinganishwa na uwezo wa wagombeaji huru wengi.

Mamlaka ya mwisho yamo mikononi mwa mpigakura, kwa hivyo raia wakome kupiga domo kuhusu dhuluma vyamani na watumie nguvu zao za kikatiba.

  • Tags

You can share this post!

KINYUA BIN KING’ORI: Wanasiasa limbukeni nchini...

Mamilioni katika hatari ya kufa njaa Kenya, Ethiopia…

T L