• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
TAHARIRI: Wakenya sharti waambiwe ukweli kuhusu kisa cha Kamiti

TAHARIRI: Wakenya sharti waambiwe ukweli kuhusu kisa cha Kamiti

Na MHARIRI

KISA cha kutoroka kwa wafungwa watatu kutoka Gereza Kuu la Kamiti kinaibua maswali mengi kuhusu uajibikaji wa vyombo vya usalama.

Idara ya Magereza imeshindwa kueleza ni vipi, watu watatu waliofungwa kwa kushiriki ugaidi walitoroka bila ya kuonekana na mtu.

Kwamba eti watatu hao walitorokea shimo ambalo hata kichwa cha binadamu hakitoshei.

Maafisa kadhaa waliokuwa zamu usiku wa tukio, walipelekwa kortini. Wanazuiliwa huku wakisubiri kufunguliwa mashtaka.

Lakini pia wapo maafisa wakuu wa idara hiyo ambao watahamishwa katika magereza mengine, huku kamishna Wycliffe Ogalo akitimuliwa.

Rais Uhuru Kenyatta kwa kumteua Brigedia Mstaafu John Kibaso Warioba, alitoa maagizo ya wazi kwamba waliohusika na kutoroka kwa wafungwa hao wachukuliwe hatua za kinidhamu.

Brigedia Warioba anapaswa kupekua na kuwaambia wakenya ukweli kuhusu yaliyojiri.

Wakati huu ambapo eneo la Upembe wa Afrika linakumbwa na machafuko na utovu wa usalama, ni makosa kwa taasisi yoyote ya ulinzi kunyamazia jambo hili.

Washukiwa hao wa ugaidi wametoroka wakati ambapo kumekuwa na taarifa za njama ya kuvamia na kulipua maeneo maarufu hapa Kenya.

Magaidi hao wameonyesha hawana mzaha kwa kulipua eneo la karibu na Bunge la Uganda.

Ingawa magaidi hawana uwezo wowote mbele ya serikali, ni muhimu kwa idara zote zinazohusika na usalama kuwasaka na kuwatia mbaroni washukiwa waliotoroka jela.

Hatua atakazochukua Brigedia Warioba zisiishie tu kwa kisa cha Kamiti.

Ni lazima ashirikiane na Inspekta Jenerali wa Polisi Hillary Mutyambai, na kufichua maovu yanayotekelezwa na maafisa wa usalama.

Haiwezekani kwa mshukiwa wa ugaidi kutoka nje ya nchi, kuvuka vizuizi vya polisi mpakani hadi kufika Nairobi au miji iliyo katikati mwa nchi bila kugunduliwa.

Kuna uwezekano mkubwa kwamba maafisa wa usalama wanaweka mbele tamaa ya pesa kuliko usalama wa wananchi.

Kama si hivyo, basi inakuwaje watu wanaozuiliwa katika vituo vya polisi wanatoroka? Kisa cha kijana Madsen Wanjala, 20, kutoroka kituo cha polisi cha Shauri Moyo hakiingii akilini mwa anayefikiria vyema.

Kisa cha punde zaidi cha washukiwa wawili kutoroka kituo cha polisi cha Kapsoya, kinazidisha wasiwasi kwa wananchi.

Ni wazi kuwa mageuzi hayahitajiki katika idara ya Magereza pekee.

You can share this post!

Tusker, Gor zaruhusiwa kutumia uga wa Nyayo

Omanyala, Kemboi kutimka katika mbio za kuinua sifa ya...

T L