• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 6:07 PM
Tusker, Gor zaruhusiwa kutumia uga wa Nyayo

Tusker, Gor zaruhusiwa kutumia uga wa Nyayo

Na CECIL ODONGO

WAWAKILISHI wa Kenya katika Kombe la Mashirikisho (CAF) Tusker na Gor Mahia sasa watatumia uga wa Kitaifa wa Nyayo katika mechi zao za nyumbani za Kombe la Mashirikisho Afrika (Caf).

Gor Mahia itapepetana na AS Otoho d’Oyo ya Congo katika raundi ya pili ya Caf huku ikicheza mechi ya mkondo wa kwanza ugenini Novemba 28 kabla ya timu hizo kurudiana hapa nchini Disemba 5.

Tusker, ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu nao, wataanza nyumbani dhidi ya CS Sfaxien ya Tunisia Novemba 28 kisha iende ugenini Disemba 5.

Timu zitakazoshinda raundi hiyo ya pili zitafuzu hatua ya makundi ya Kombe la Mashirikisho ambapo kila timu hupokezwa Sh27 milioni.

Hapo jana Jumatano, Mkurugenzi wa Michezo wa Gor Mahia Lordvick Aduda alieleza Taifa Leo kuwa wamepata barua kutoka kwa Caf ikiwaruhusu watumie uga wa Nyayo kwa mechi dhidi ya AS Otoho d’Oyo.

“Caf imeturuhusu tutumie uga wa Nyayo kwa mechi yetu dhidi ya As Otoho d’Oyo ila ikasisitiza kuwa tukitinga hatua ya makundi basi lazima tutafute uwanja mbadala iwapo Nyayo haitakuwa imekaratabiwa,” akasema Aduda.

“Ni nafuu kwetu kwa sababu tungetumia uwanja wa Benjamin Mkapa nchini Tanzania, gharama ingekuwa juu na hatungeandamana na mashabiki wetu,” akaongeza.

CAF mnamo Oktoba 17 iliandikia Shirikisho la Soka Nchini (FKF) ikiharamisha matumizi ya uga wa Nyayo katika kuandaa mechi za kimataifa na Bara za Afrika.

Katibu wa Gor Mahia Sam Ochola naye aliandikia FKF mnamo Novemba akiirai iombe Caf iruhusu mechi hiyo isakatwe Nyayo.

Afisa Mkuu Mtendaji wa Tusker Charles Obiny naye alisema kwa kuwa Gor imeruhusiwa kutumia uwanja huo wao pia watautumia japo hawakuandikia Caf.

K’Ogalo ilimbandua Al Ahly Merowe kwa jumla ya 3-1 kwa mkondo wa kwanza ila wakakosa mpinzani mkondo wa pili baada ya timu hiyo kukosa kufika uwanjani.

Tusker nayo ililemewa 5-0 na Zamalek ya Misri kwenye raundi ya kwanza japo iliifurusha Arta Solar 7 ya Djibouti kwenye hatua ya mwondoano kupitia jumla ya magoli 4-1.

You can share this post!

Pigo kwa ‘mpango wa kando’ Uhuru akisaini...

TAHARIRI: Wakenya sharti waambiwe ukweli kuhusu kisa cha...

T L