• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 7:15 PM
WANDERI KAMAU: Agizo la Gachagua halitatatua athari za pombe Mlima Kenya

WANDERI KAMAU: Agizo la Gachagua halitatatua athari za pombe Mlima Kenya

NA WANDERI KAMAU

HADI sasa, ingali kubainika kuhusu ikiwa aliyekuwa Chansela wa Ujerumani kati ya 1933 na 1945, Adolf Hitler, alitimiza lengo lake la “kuwaangamiza kabisa” Wayahudi alipoanzisha Vita Vikuu vya Pili vya Dunia, vilivyodumu kati ya 1939 na 1945.

Kuna nadharia mseto. Kwa baadhi ya wasomi, Hitler alitimiza lengo hilo, ijapokuwa baadhi yao wanasema hakutimiza.
Bila shaka, uongozi wa Adolf Hitler ni miongoni mwa nyakati ambazo zimetajwa kuwa “ngumu zaidi kwa mwanadamu” tangu uumba wa dunia.

Ni wakati ambapo mwanadamu alimgeukia mwanadamu mwenzake kwa msingi wa asili yake, tabaka lake, dini yake na mwegemeo wake wa kisiasa.

Kupitia sera zake za kibaguzi, Hitler alisababisha maafa ya zaidi ya Wayahudi milioni sita barani Ulaya.

Baada ya vita hivyo kukamilika, mbegu ya chuki aliyoipanda Hitler ilionekana kuzagaa na kuenea kote kote duniani.

Mbegu hiyo iliendeshwa na mashambulio ya bomu za nyuklia yaliyotekelezwa na Amerika katika miji ya Hiroshima na Nagasaki nchini Japan mnamo Agosti 6, 1945.

Matukio mengine yaliyoonyesha ukatili wa mwanadamu dhidi ya mwanadamu mwenzake ni ubaguzi wa rangi ulioendeshwa na Weupe dhidi ya watu Weusi nchini Amerika, ambapo upeo wake ulikuwa ni mauaji ya mwanaharakati Martin Luther King mnamo 1963.

Ukatili mwingine ulishuhudiwa katika mataifa tofauti barani Afrika, ambayo yalikuwa yakijaribu kujikomboa kutoka minyororo ya ukoloni.

Baadhi ya mataifa hayo ni Kenya, Algeria, Morocco, Afrika Kusini, Angola, Tanzania kati ya mengine.

Nchini Kenya, Waingereza walitumia karibu nguvu zote za kijeshi kukabiliana na wapiganaji wa Mau Mau—wengi wao wakitoka katika jamii za Agikuyu, Aembu na Ameru.

Nchini Afrika Kusini, dunia nzima ilitazama jinsi Wazungu waliendesha ukatili uliopita mipaka dhidi ya Waafrika.

Kando na kuwabagua katika nyanja tofauti muhimu kama vile elimu, utawala huo pia uliwatesa na kuwafunga gerezani viongozi maarufu wa harakati za ukombozi kama vile Nelson Mandela, Walter Sisulu, Oliver Tambo kati ya wengine.

Urejeleo huu wote unaashiria jinsi mwanadamu anaweza kutumia hila kufikia malengo yake, bila kujali ikiwa anamwangamiza mwanadamu mwenzake au la.

Katika eneo la Mlima Kenya, tatizo la matumizi ya mihadarati linafanana na vile ubaguzi wa rangi ulivyokolea katika mataifa kama Amerika.

Ni saratani inayoonekana kukosa tiba. Mnamo Julai 2015, Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta aliagiza msako mkali dhidi ya watengezaji pombe haramu katika eneo hilo, ijapokuwa juhudi zake hazikufaulu.

Mnamo Alhamisi, Naibu Rais Rigathi Gachagua alitoa agizo kama hilo, alipohutubu katika Kaunti ya Murang’a. Ukweli ni kuwa, maonyo na maagizo makali hayatamaliza tatizo hilo Mlimani. La hasha!

Sababu ni kuwa, baadhi ya wale wanaotengeneza pombe hizo hatari ni washirika wa karibu wa viongozi walio mamlakani. Ni vipi tena viongozi watawapiga vita “wafadhili wao”?

Mkakati mpya unahitajika kukabili tatizo hilo. La sivyo, litabaki kuwa saratani isiyo tiba daima.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Waisraeli sasa kupewa bunduki ili wajilinde

Kijana mjasiriamali atangaza nia ya kufuata nyayo za Ruto

T L