• Nairobi
  • Last Updated April 17th, 2024 6:55 PM
Waisraeli sasa kupewa bunduki ili wajilinde

Waisraeli sasa kupewa bunduki ili wajilinde

NA MASHARIKI

JERUSALEM, ISRAELI

WAZIRI Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu ametangaza mpango wa kurahisisha taratibu za Waisraeli kumiliki bunduki kutokana na mapigano yanayoendelea kuongezeka baina ya taifa hilo na Wapalestina.

Hata hivyo, tayari hatua hiyo imekosolewa kama ambayo huenda ikaongeza mapigano yanayoendelea.

Netanyahu alitangaza mpango huo Jumamosi, baada ya kufanya mkutano kuhusu hali ya usalama nchini humo na mawaziri wanaosimamia masuala ya usalama.

Mkutano huo unafuatia visa kadhaa vya ufyatulianaji risasi, vinayojumuisha shambulio katika eneo la Mashariki mwa Jerusalem.

Watu saba waliuawa kwenye shambulio hilo lililofanyika katika eneo hilo Ijumaa, nje ya hekalu moja.

Mashambulio hayo yalifanyika katika mwezi ambao kumekuwa na mivutano mikubwa baina ya pande hizo mbili. Awali, vikosi vya Israeli vilivamia mji wa Jenin, ulio katika eneo la West Bank, na kuwaua Wapalestina tisa.

Katika mashambulio yote yaliyotokea mwezi huu, vikosi vya Israeli vimewaua jumla ya Wapalestina 32.

Kwa muda mrefu, Israeli haijatekeleza mashambulio ya kiwango kama hicho mjini Jenin, ijapokuwa vikosi vyake vilikuwa vimeongeza operesheni yake katika eneo la West Bank mwaka 2022, ambapo karibu Wapalestina 200 waliuawa.

Mnamo Jumamosi, Netanyahu aliahidi kuongeza kasi ya utoaji vibali vya umiliki wa bunduki miongoni mwa raia nchini humo na “kukusanya silaha haramu”.

Aliongeza kuwa makazi ya watu wanaotuhumiwa kuwashambulia raia au kuwaunga mkono Wapalestina yatazungukwa na kubomolewa mara moja “kama adhabu ya kuunga mkono ugaidi”.

Kwenye taarifa, afisi yake ilisema kuwa misaada ya kifedha ambayo watu hao wamekuwa wakipokea kutoka kwa serikali pia itafutiliwa mbali.

Pia, aliahidi kuchukua hatua mpya “kuwapa nguvu” Waisraeli wanaoishi katika eneo inalokalia la West Bank ijapokuwa hakutoa maelezo zaidi.

Tayari, polisi nchini humo wamewaagiza raia ambao wana vibali vya kumiliki bunduki kuanza kuzibeba wanapoendelea na shughuli zao.

“Ijapokuwa Netanyahu anawarai Waisraeli kutochukua sheria mikononi mwao, anawapa silaha raia anaowapa ujumbe huo,” akasema afisa mmoja wa shirika la kutetea haki za binadamu katika eneo la Mashariki ya Kati.

Afisa huyo alitaja hatua ya Netanyahu kama “adhabu ya pamoja dhidi ya familia za Kipalestina” na “ukiukaji wa wazi wa haki za binadamu”.

Wadadisi wanasema kuna uwezekano mkubwa hatua hiyo kuongeza taharuki na mashambulio baina ya pande hizo mbili.

  • Tags

You can share this post!

KEN OKANIWA: Miaka 60 ya ushirikiano wa Kenya na Japan...

WANDERI KAMAU: Agizo la Gachagua halitatatua athari za...

T L