• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 9:01 PM
WANDERI KAMAU: Amerika ikome kufumbia macho uozo unaoikabili

WANDERI KAMAU: Amerika ikome kufumbia macho uozo unaoikabili

NA WANDERI KAMAU

MNAMO Ijumaa, serikali ya Amerika ilitoa tahadhari ya usafiri kwa raia wake nchini Kenya kutokana na “tishio la shambulio la ugaidi”.

Amerika iliwaonya raia wake kutosafiri katika baadhi ya maeneo ya Pwani na kaunti zilizo karibu na mpaka wa Kenya na Somalia, kwani huenda “yakakumbwa na mashambulio ya kigaidia wakati wowote”.

Vilevile, iliwatahadharisha kutosafiri au kutembelea maeneo yaliyo katika kaunti za Turkana na Nairobi kutokana na tishio la kutekwa nyara.

Bila shaka, hii si mara ya kwanza kwa Amerika kutoa tahadhari kama hizo. Imekuwa ni mazoea yake.

Hata hivyo, kile huwa kinashtua ni kwamba haijawahi kutoa tahadhari kama hizo ikiwonya raia wake wasisafiri katika nchi kama Uingereza, China, Ubelgiji, Ujerumani au mataifa mengine mengi yaliyostawi kiuchumi.

Tahadhari zake hulenga tu nchi maskini na zenye chumi za kadri barani Afrika, Asia au Mashariki ya Kati.

Swali linaloibuka ni: Ni katika mataifa hayo pekee ambapo vitendo vya “ugaidi” hufanyika, kulingana na fasiri ya Amerika na mataifa washirika wake?

Jumanne, mtu aliyekuwa na bunduki aliwaua watu 18 katika shule moja katika jimbo la Texas, Amerika, kwa kuwafyatulia risasi.

Katika tukio hilo la kusikitisha, kati ya waliouawa ni wanafunzi wachanga na walimu wao.

Kinaya ni kuwa, badala ya Amerika kuendeleza juhudi zake za kutatua ongezeko la visa vya watu kuuana kwa kufyatuliana risasi nchini mwake, inaanza kutoa “tahadhari” za usafiri kwa raia wake katika mataifa maskini.

Kwanza, huu ni unafiki mkubwa kwa utawala wa Rais Joe Biden, kuwa hata baada ya kutoa ahadi ya mwanzo mpya wa kiutawala nchini humo, bado anaendeleza sera za kibaguzi zilizokuwa zikiendeshwa na tawala zilizomtangulia.

Msingi wa tawala za marais kama George Bush II na Donald Trump ulikuwa ubaguzi na dhuluma dhidi ya watu Weusi kwa jumla.

Ni wakati wa utawala wa Bush (2000-2008) ambapo chuki kati ya Amerika na jumuiya ya Kiarabu kote duniani ilifikia upeo wa juu zaidi.

Ni katika enzi hiyo ambapo Amerika ilianza mashambulio makali katika nchi za Iraq, Afghanistan, Pakistan na Lebanon kukabiliana na makundi ya kigaidi kama vile Al-Qaeda na Hizbollah.

Nchini Ufilipino, Amerika ilishirikiana na serikali ya taifa hilo kukabiliana na kundi la Abu Sayaf, lililodaiwa kuendeleza itikadi kali za Kiislamu.

Bila shaka, vitendo hivyo ndivyo vilivyojenga chuki kali kati ya Bush na jamii ya Kiarabu na Kiislamu kote duniani, kwani alionekana kuwalenga kwenye vita hivyo.

Kwa upande wake, Trump alilaumiwa kwa kujenga chuki kati ya Waamerika Weusi na Weupe, hali inayoonekana kuwa mojawapo ya sababu zilizomfanya kushindwa na Rais Biden kwenye uchaguzi wa Novemba 2020.

Wito mkuu kwa Rais Biden ni kutofufua chuki mpya kati ya utawala wake na mataifa maskini, kwa kufumbia macho maovu yanayoendelea Amerika na kupitisha lawama kwa nchi hizo.Amerika ikubali maovu yake kabla ya kuyaona ya mataifa mengine.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Wanasiasa watumie kampeni kuelewa matatizo ya raia

WANTO WARUI: Huenda mtihani wa mfumo wa CBC Gredi ya 6,...

T L